July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Jeshi hili la polisi livunjwe

Rais Jakaya Kikwete akimuapisha IGP, Ernest Mangu

Spread the love

JANUARI mwaka huu, baadhi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri, walipendekeza kwa serikali jeshi la Polisi livunjwe na kuundwa upya. Niliyapenda maoni haya, ijapokuwa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hawakuyapenda.

Lakini mimi kama raia wa Jamhuri ya Muungano na mpenda amani, ninasimama na wabunge waliotaka jeshi hili la sasa livunjwe. Sababu ni hizi:

Kwanza, kitengo cha intelijensia ya polisi imepwaya. Wahalifu wanapanga mikakati na uhalifu unafanikiwa.

Ushahidi ni vituo vya polisi kutekwa; kuvamiwa na watu wasiojulikana, kuua askari; kuiba bunduki na risasi na kisha kutokomea kusikojulikana.

Matukio ya aina hii ni mengi. Kwa mfano, 7 Septemba 2014, kituo kikuu cha polisi wilayani Bukombe, mkoani Geita, kilivamiwa na askari wawili kuuawa na kisha bunduki 10 kuibwa.

Aidha, 21 Januari 2015, watu walioitwa majambazi walivamia kituo cha polisi cha Ikwiriri mkoani Pwani. Askari wawili wa jeshi hilo waliuliwa na silaha kuibwa.

Matukio mengine ni yale ya 26 Januari 2015 katika mtaa wa barabara ya 4 huko Tanga, ambako askari wawili – HV 507 PC, Mwalimu na G 369 PC Mansour – waliuawa wakiwa kazini.

Wakiwa katika doria kwa kutumia pikipiki, walivamiwa na wanaoitwa na serikali, “watu wasiojulikana,” wakapigwa na kisha wakanyanganywa bunduki mbili aina ya Sub Machine Gun (SMG).

Tarehe 1 Februari 2015, watu walioitwa majambazi walivamia kituo kidogo cha Polisi Mngeta, wilayani Kilombero. Waliiba bunduki aina ya SMG iliyokuwa na risasi 30.

Kwa matukio haya, kama intelijensia ya polisi haina uwezo wa kubaini mikakati na mipango ya kiuhalifu dhidi yake yenyewe, yawezaje kubaini uhalifu unaopangwa dhidi ya wananchi?

Pili, kuundwa upya kwa jeshi la polisi, kunatokana na uhasama uliopo kati ya askari polisi na wananchi. Ulinzi na usalama wa nchi ni kazi ya watu wote.

Lakini kuna uhasama hasa wa kulipiza visasi kati ya polisi na wananchi. Mifano ni mingi.

Kauli za Paul Chagonja, mmoja wa maofisa wa ngazi ya juu ndani ya jeshi hilo, nazo zinathibitisha hili.

Akiwa katika mazishi ya mmoja wa askari wa jeshi la polisi, huko wilayani Karagwe, 30 Julai 2011, Chagonja alinukuliwa akisema, kati ya mwaka 2005 na 2011, zaidi ya askari polisi 25 waliuawa na wananchi.

Tarehe 24 Novemba 2012, wananchi wilayani Bukombe mkoani Geita, walikivamia kituo cha polisi cha Ushirombo kwa lengo la kukichoma moto. Hii ni baada ya askari kutoka kituoni hapo aliyetajwa kwa jina la Manase kutuhumiwa kumuua Bw. Rashidi Juma.

Tarehe 15 Desemba 2012, wananchi katika kijiji cha Mugoma, kata ya Mugoma tarafa ya Kanazi wilayani Ngara, waliwaua polisi wawili: E. 579 Koplo Paschal na H. 429 Konstebo Alexanda.

Askari hao walituhumiwa na wananchi kumuua fundi pikipiki, Said Mukonikoni.

Tarehe 24 Januari 2013, wananchi wa Kibiti mkoani Pwani, walichoma nyumba nane za polisi baada ya kuwatuhumu askari hao kumuua Hamisi Mpondi aliyekuwa ametuhumiwa na polisi kuuza bangi.

Katika purukushani hizo askari polisi walipoteza mali zao na polisi mmoja PC Dominick alipoteza maisha.

Tarehe 18 Septemba 2014, askari watatu – G7351 PC Ramadhan; WP 10399 PC Felista na H 3484 PC Respicus, walijeruhiwa kwa bomu lililorushwa na watu ambao hawakufahamika na jeshi hilo. Tukio hili lilitokea Mabatini katika manispaa ya Songea.

Tarehe 11Februari 2015, askari polisi aliyekuwa katika doria kwa kutumia pikipiki alijeruhiwa na waendesha pikipiki kwa kupigwa chupa baada ya kumkamata mwenzao aliyekuwa na matatizo katika pikipiki yake.

Ni jambo la kushangaza kuona baadhi ya viongozi wakishindwa kubaini chanzo cha kutoaminiana kati ya wananchi na polisi.

Tatu, jingine ambalo limenisukuma kupendekeza jeshi la polisi livunjwe, ni kule kushindwa kupambana na gonjwa sugu la rushwa. Kila tafiti zinazotolewa kuhusu rushwa zinaonesha jeshi hili linaongozwa kwa kuendekeza matendo hayo.

Kwa mfano, taarifa ya ‘East Africa Bribery Index’ ya mwaka 2013 inaonyesha jeshi la polisi nchini ndiyo taasisi kwa asilimia 50 kwa vitendo vya rushwa.

Kuna wakati kumeripotiwa kuwapo mapigano ya risasi na hata mauaji kati ya polisi na jeshi kwa sababu ya kunyimana mgawo wa rushwa.

Mfano hao, ni tukio la tarehe 14 Februari 2012, katika eneo la Mtoni Kijichi jijini Dar es Salaam. Katika tukio hili, askari polisi waliokuwa doria, F. 8588 PC Rajabu na G. 1845 PC Samwel, walimpiga risasi ya ubavuni na kumjeruhi askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), MT 78975 PET Gabriel Mwamagemo.

Kisa cha Mwamagemo kupigwa risasi, ni kuwanyima askari hao rushwa ya Sh. 5,000 (elfu tano).

Fedha hizi walitaka walipwe kama fidia ya kumkamata mwendesha bodaboda aliyekuwa amebeba mifuko ya saruji mali ya dada yake Mwamagemo kwa madai kuwa haikuwa na risiti ya manunuzi.

Mnamo Machi 2013 mkazi wa kata ya usinge wilayani Kaliua Ngidingi Lusumisha (67) alibambikiwa kesi ya kukutwa na fuvu la binadamu na kisha kuombwa rushwa ya Sh. 200, 000 (laki mbili) ili asikamatwe na kupelekwa mahakamani.

Yeye alisisitiza kuwa fuvu hilo walikuja nalo polisi na kisha kuliweka kwenye zizi lake la ng’ombe.

Tukio lingine la kubambikiwa fuvu la binadamu liliripotiwa katika eneo la Dumila, wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, mwaka 2011.

Ni pale askari polisi watatu walipoweka fuvu hilo kwenye uvungu wa gari la Samson Mura na kisha kumtaka kulipa kiasi cha Sh. 20 milioni ili wasimkamate na kumfikisha mahakamani.

Matukio haya na mengine, ni uthibitisho tosha kuwa jeshi la polisi limeshindwa kazi na wananchi wamelichoka jeshi hilo.

Hivyo basi, siyo vema kuendelea kuwa na jeshi la aina hii. Bila kukijenga upya chombo hiki, hakuna shaka kuwa huko tuendako ni giza.

Kuna umuhimu mkubwa wa jeshi hili kuvunjwa ili kuliokoa taifa na machafuko.

Mwandishi wa makala hii, Christian Mwesiga, amejitambulisha kuwa msomaji wa gazeti hili. Anapatikana kwa simu Na. 0756267870 na 0652845836. imeil: chrismwesiga@Gmail.com

error: Content is protected !!