WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa amewataka wakuu wa mikoa kutekeleza maagizo yaliyotolewa na kamati ya mawaziri nane, kwa ajili ya kutatua migogoro ya ardhi katika maeneo yao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).
Silaa ametoa agizo hilo leo tarehe 6 Septemba 2023, bungeni jijini Dodoma, akijibu swali la Mbunge Viti Maalum, Condester Sichalwe, lililohoji mpango wa serikali katika kumaliza migogoro ya ardhi iliyoko katika Kata ya Kapele, mkoani Songwe.
“Serikali imepinga na Serikali kupitia kamati ya mawaziri nane ilishafanya utatuzi wa migogoro ya ardhi kwenye vijiji 975 na naomba kutumia fursa hii kuwakumbusha wakuu wa mikoa nchi nzima kuendelea na utekelezaji wa maagizo ya baraza la mawaziri,” amesema Silaa.
Mbali na agizo hilo, Silaa amesema atafanya ziara nchi nzima ili kuhakikisha maagizo ya kamati hiyo ya mawaziri yanafanyiwa kazi.
Awali, Sichalwe akiuliza swali lake alisema “lini wizara itaingia kati na kutusaidia migogoro ya ardhi iliyoko ndani ya Kata ya Kapele? Kwa kufuatilia watu wamehodhi na kupora maeneo ya wananchi kinyume na taratibu na wengine kuwa na hati za uongo kwa kigezo wameagizwa na wakubwa huko juu.”
Leave a comment