September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Jengeni tabia ya kupima presha ya macho – CCBRT

Mgonjwa wa macho akipata vipimo

Spread the love

WATANZANIA wamewatakiwa kuwa na utaratibu wa kupima presha ya macho angalau mara moja kwa mwaka, pia kufika hospitali kupata matibabu ya macho kwa wakati. Anaripoti Hamis Mguta …  (endelea).

Hayo yameelezwa na Dk. Cyprian Ntomoka, Daktari Bingwa wa Macho katika Hospitali ya CCBRT, wakati wa maadhimisho ya miaka 25 ya hospitali hiyo.

Dk. Ntomoka amesema, wagonjwa wengi wa macho wanafika hospitali wakiwa katika hali mbaya, huku presha ikifika 50 na kupelekea changamoto katika kuwatibu wakati kwa kawaida inapaswa isizidi 20.

“Presha ya macho ni ugonjwa ambao ni mgumu katika matibabu yake, mtu anakuja na presha imefika 50 au 60, kinachofuata jicho linaanza kuuma, unakuta jicho limepoteza kuona, matokeo yake mgonjwa anakuja na jicho ambalo halioni na pia linamuuma,” amesema.

Amesema, zamani watu walikuwa hawana uelewa na kusema wamerogwa baada ya kupata matatizo ya macho, hivyo hospitali hiyo imeongeza muamko wa watu juu ya magonjwa ya macho.

“CCBRT imefanya kazi kubwa sana kwasababu, unajua mtaji mkubwa wa shetani ni ujinga, sasa kulikuwa na ujinga mwingi kwenye vichwa vya watu wakawa wanakaa nyumbani bila matibabu, kilichobaki sio watu kuja ni kuja kwa wakati,” amesema.

Amesema, watu wengi wanadhani ugonjwa wa macho unatibiwa na miwani, hivyo miwani imekuwa ni adui wa macho kwa kudhani watu wakitumia miwani, macho yataingia ndani au kutoka jambo ambalo si la kweli.

Brenda Msangi, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa CCBRT amesema, licha ya kuwa hospitali hiyo inatibu magonjwa mengi ikiwemo Fistula, Mdomo Wazi na hata Mguu Vifundo na magonjwa mengine, bado asilimia 70 ya wagonjwa wanaofika kwa matibabu ni wa macho.

“Siku ya leo tumeitumia kwa kuwatembeza waandishi wa habari katika maeneo mbalimbali ya hospitali yetu, ili kuielewa taasisi hii vizuri kufuatia miaka 25 tangu kuanzishwa kwake.

“…lakini tunawasihi wagonjwa ambao wanafika kwa huduma zingine kama mguu vifundo wanashauriwa wafike mapema ili kusaidia matibabu yaende vizuri,” amesema.

Msangi amesema, takribani kila mwaka wanapata wagonjwa wapya 100,000 na kwamba, wameweza kutengeneza ujuzi kwa wataalamu wengine wakiwemo wa fistula, amnapo mwaka huu wamepata timu kutoka nchini Yemen waliofika kujifunza kuhusu ugonjwa wa fistula.

error: Content is protected !!