ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera, Benson Bagonza na mwandishi wa habari mkongwe nchini, Jenerali Ulimwengu, wameonesha njia kuhusu suluhu ya madai ya katiba mpya. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza katika uzinduzi wa kitabu chake cha Rai ya Jenerali, leo Jumanne tarehe 21 Septemba 2021, jijini Mwanza, Ulimwengu ameshauri mabadiliko ya katiba yafanyike, ili kuziba mapungufu yake.
Ulimwengu amesema kuwa, mapungufu ya katiba yanayonekana kila siku kutokana na matumizi yake, hivyo kama yataonekana inatakiwa marekebisho yafanyike.
“Ni kweli na mimi huwa nasema katiba ni kitu ambacho kinaishi, mnaishi nacho siku zote na kila siku unapokitumia kitakuonesha kina mapungufu katika maeneo fulani fulani,” amesema Ulimwengu na kuongeza:
“Na hayo mapungufu yanaweza kuwa makubwa au madogo, kama madogo yanahitaji mabadiliko madogo madogo. Kama makubwa yanahitaji over roll na ifanyike.”
Naye Askofu Bagonza, amesema ili katiba mpya ipatikane wanaohitaji mabadiliko hayo waibembeleze Serikali iliyopo madarakani.
“Hakuna uwezekano wa kupata katiba mpya nje ya CCM na hakuna uwezekano wa kuiondoa CCM bila katiba mpya, ni sawa na kuku na yai, kipi kina anza kuku au yai? ” amesema Askofu Bagonza na kuongeza:
“Nitalisema hili si kwa sababu nachukia jambo lolote, ninachotaka kusema inaonekana upinzani wa katiba uko ndani ya chama hicho. Ukitaka katiba mpya ni lazima ama uwabembeleze hawa au uwalazimishe.”
Madai ya katiba mpya yaliibuliwa hivi karibuni na baadhi ya vyama vya siasa vya upinzani, hasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGO’s), wakidai katiba iliyopo ina mapungufu.
Hata hivyo, Rais Samia Suluhu Hassan aliwaomba watu wanaotaka katiba mpya wampe muda wa kuijenga nchi kiuchumi.
Leave a comment