VYOMBO vya ulinzi na usalama nchini Tanzania, vimemhakikishia ulinzi Rais wa nchi hiyo, Samia Suluhu Hassan. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Ahadi hiyo imetolewa leo Ijumaa tarehe 26 Machi 2021, Mkuu wa Majeshi, Jenerali Venance Mabeyo, katika Misa Takatifu ya mazishi ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Pombe Magufuli, iliyofanyika Uwanja wa Mpira wa Magufuli, Chato mkoani Geita.
” Vyombo vya ulinzi na usalama, vinapenda kukuhakikishia kuwa ulinzi wa nchi na mipaka yake ni salama na kwamba vitaendelea kukulinda wewe kama rais, kukutii kama Amiri Jeshi Mkuu na kutekeleza wajibu wake kama ilivyoanishwa kwenye katiba,” amesema Jenerali Mabeyo.
Amesisitiza “vyombo vya ulinzi na usalama vinakuhakikishia utiifu, uadilifu na uaminifu mkubwa kwako rais na Amiri Jeshi Mkuu kama ilivyo mila na desturi ya jeshi letu.”
Mkuu huyo wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, amemhakikishia Rais Samia kwamba hali ya nchi ni tulivu, na mipaka ya nchi iko salama.
https://www.youtube.com/watch?v=Nu5TFZVfqTQ
“Tunakupongeza kwa dhati kwa kuapishwa kwako kuwa Rais wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu kwa mujibu wa katiba, utaendelea kuitwa Amiri Jeshi Mkuu na sio Amirat. Hali ilivyo nchini ni tulivu na mipaka yote iko salama,” amesema Mabeyo.
Samia aliyekuwa Makamu wa Rais wa Tanzania, ameapishwa kuwa Rais wa Tanzania tarehe 19 Machi 2021, Ikulu jijini Dar es Salaam, akichukua mikoba ya Dk. Magufuli, aliyefariki dunia akiwa madarakani.
Dk. Magufuli alifariki dunia tarehe 17 Machi 2021, kwenye Hospitali ya Mzena, Makumbusho mkoani Dar es Salaam, alikokuwa anapatiwa matibabu ya ugonjwa wa mfumo wa umeme wa moyo.
Mwanasiasa huyo alifikwa na umauti miezi minne tangu alipoapishwa kuendelea na muhula wake wa mwisho katika Serikali ya awamu ya tano, tarehe 5 Novemba 2020, baada ya kushinda kiti cha urais wa Tanzania katika uchaguzi mkuu.
Dk. Magufuli aliiongoza Tanzania kwa miaka mitano na miezi mitano mfululizo (2015-2021), na mwili wake unatarajiwa kuzikwa kijijini kwao Chato mkoani Geita.
Leave a comment