January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Jenerali Gilbert Diendere kuongoza Burkina Faso

Spread the love

BAADA ya mapinduzi nchini Burkina Faso, walinzi wa Rais wamemtangaza Jenerali Gilbert Diendere ambaye alikuwa rafiki wa karibu wa Rais Blaise Compaore, kuwa kiongozi mpya wa taifa hilo.

Taarifa iliyotolewa na walinzi hao imesema Diendere, aliyekuwa mkuu wa majeshi chini ya Compaore, ndiye atakayekuwa rais mpya.

Tangazo la awali kupitia runinga ya taifa lilisema mashauriano yangefanyika kuunda serikali mpya ya mpito ambayo ingeandaa “uchaguzi wa amani na wa kuhusisha wote”.

Spika wa bunge la mpito Cheriff Sy amesema hayo ni “mapinduzi ya serikali”. Hayo yamejiri huku ufyatulianaji wa risasi ukiripotiwa jiji kuu la Ouagadougou. Rais Francois Hollande alishutumu hatua ya walinzi hao wa rais ya kupindua serikali.

Walinzi hao wanadaiwa kufyatulia risasi waandamanaji waliokuwa wakiandamana Ouagadougou kupinga hatua ya wanajeshi hao na baadhi wamekamatwa, ripoti zinasema.

Makao makuu ya chama cha Compaore cha Congress for Democracy and Progress (CDP) yalivamiwa na waandamanaji na kuporwa, baada ya habari za mapinduzi hayo kuenea.

Hollande ameitisha kuachiliwa mara moja kwa Kaimu Rais Michel Kafando na Waziri Mkuu Isaac Zida, waliozuiliwa wakiongoza mkutano wa baraza la mawaziri ikulu ya rais Jumatano.

Serikali yao ya mpito ilitarajiwa kukabidhi mamlaka kwa serikali ambayo ingechaguliwa kwenye uchaguzi mkuu Oktoba 11 mwaka huu.

Rais Compaore aliondolewa madarakani baada ya maandamano ya raia mwaka jana na kwa sasa anaishi uhamishoni. Alikuwa ameongoza taifa hilo kwa miaka 27.

error: Content is protected !!