June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Jecha hajiwezi kwa CCM

Spread the love

UFUATILIAJI wangu uliosaidiwa na watoa taarifa serikalini na kwengineko, unanipa jeuri ya kuamini kuwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanamdhibiti Jecha Salim Jecha anayeendelea kuitwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC). Anaandika Jabir Idrisa.

Madhumuni yao ni kumsimamia atangaze wanachokitaka wao, huku viongozi haohao wakijidai Tume ya Uchaguzi ni huru isiyoingiliwa na mtu yeyote.

Wanamaana kuwa wao viongozi wa CCM pamoja na watendaji wa serikali wanaowatumia kutimiza azma zao chafu, si watu isipokuwa mashetani.

Niliwahi kuandika kwamba nilimpa Jecha hongera-pole kwa kuteuliwa kuongoza Tume muda mfupi baada ya kutajwa 2013. Nilimwambia hiyo kazi itamshinda. Nilijua na namjua.

Hajiwezi kimapenzi juu ya CCM; wakati huo si alishatafuta tiketi ya chama hicho kugombea ubunge Jimbo la Amani, Unguja, katika uchaguzi mkuu 2010? Anajizongoa vipi hapo?

Ni kwa sababu tu utawala wa sheria unakanyagwa ili kuruhusu wakubwa wa CCM kufika watakapo, lakini Jecha angekuwa kitanzini kwa alichokifanya 28 Oktoba akiwa anakokujua huku akitelekeza wenzake katika Tume waliokuwa kikaoni ukumbi wa Salama katika Hoteli ya Bwawani kilipokuwa kituo cha matangazo ya uchaguzi.

Hastahili kuonewa huruma. Amehujumu haki ya wananchi kuamua watakacho, ameitia hasara serikali iliyotumia mabilioni ya shilingi (inatajwa Sh. 7 bilioni hivi) kugharamia uchaguzi.

Jecha ni mhalifu anayesubiri siku ili ashitakiwe. Baada ya hapo, kwa sababu ushahidi wa uhalifu aliotenda hautaki tochi, kitakachofata ni kuadhibiwa na mahakama. Kiwango cha adhabu atakiamua hakimu lakini gerezani itakuwa makazi yake.

Angalia sasa unayetamba ni Mzanzibari au wewe Mtanzania wa upande mmoja unaounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, unapokuwa na serikali inayolinda mhalifu mkubwa kama huyu, unajisikiaje? Twende mbele.

Chumbani wanawaweka, wahalifu wasishikwe, kama vile ni kubaka, sheria isisimame, bali siku watataka, ukweli udhihirike. Hapo patakuwa Jecha, dubwana, na wote walokosea; zombi nao watajua, wafisadi tasogea, na roho zikapasuke, hela dhuluma patokwe. Eti nini? Dhuluma ikome.

Nchi ya nani? Watu. Watu ni nani? Umma. Umma ni nani? Mkusanyiko wa wanadamu ndani ya nchi yao kwa ajili ya maslahi yao, wao kama raia, na nchi yao – Zanzibar. Hapo pamekaa sawasawa. Panasomeka!

Basi Wazenjibari watu karimu, tena karimu walotulia, hawataki upotevu, si kwa hili wala lile, milele wataka sawa, haki, hishima, imani na uadili kusawiri. Hao ndio watu wetu, ndio watu wetu. Wetu kwelikweli. Wetu!

Jecha ni mhalifu kama walivyo askari wa serikali wanaojifunika vitambaa usoni na kuzunguka mitaa kwa gari za serikali zikiwemo za KM (Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo) na MF (Kikosi cha Mafunzo).

Wanapiga wananchi, wanaharibu mali zao, wakipambana na vitu visivyosema kama bendera za Chama cha Wananchi (CUF), milingoti, mabenchi katika barza zao na sasa kuteketeza mikarafuu shambani.

Mhalifu kama walivyo watendaji serikalini wanaoiba fedha za wananchi kwa visingizio vya kuandaa uchaguzi wa marudio, uteuzi wa watendaji usonjia wala nia, na kuongezea nchi majeshi kama vile imeingia vitani. Wafanyao au kufanikisha hayo, wote ni wahalifu tu kama Jecha.

Huu ndio ukweli ninaoujua. Wanasheria – nakusudia wale wanaojiheshimu kama wanataaluma wa kusaidia jamii wala sio waharibifu wanaotumikia majizi na mavizaji demokrasia – wanajua hivyohivyo hakuwa na mamlaka ya kisheria.

Kwanza hakuna kifungu cha sheria, pia hakuna kikao kilichotangulia maamuzi aliyofanya. Haramu haramu haramu.

Siku hizi vikao vya Tume ya Uchaguzi Zanzibar haviendi kikawaida. Hakuna majadiliano endelevu, bali kufanyia kazi fikra za wanasiasa waovu zilizofikishwa na mateka wao kimaslahi.

Tume imekuwa ikipiga muhuri kuridhia yale yanayokidhi matakwa ya CCM na Serikali, vinavyoshikwa na walewale wanaomlinda Jecha na wanaomuelekeza Mkurugenzi wa Tume.

Mtendaji mmoja anasema hakuna mjadala wenye mantiki na akili, vikao huendeshwa kimabavu. Utaratibu wa kuridhia mambo kwa kupiga kura ndio staili ya kupitisha maamuzi, sio tena makamishna kuamua baada ya kuangalia mantiki ya jambo lililowekwa mezani kufikiriwa.

Ndugu yangu siku hizi kinachofikishwa lazima kipigiwe kura. Wanajua (wakubwa) itasimama 3-3 na Jecha akitia yake, lazima tu kura itawalalia Makamu Mwenyekiti, Jaji Abdulhakim Ameir Issa, Nassor Khamis Mohamed na Ayoub Bakari Hamad.

Hawa makamishna wawili wa mwisho, wanatokana na uteuzi uliofanywa kwa mashauriano na kiongozi wa upinzani.

Si hasha ukasikia bado inaaminishwa eti uchaguzi uliharibika na ukafutwa kihalali. Uhalali wa kisheria wa ufutwaji uchaguzi, ukajengwa baada ya ufutwaji. Mzaha, unafutaje uchaguzi wa wananchi, ndipo utafute ridhaa ya Tume. Umajununi mtupu.

Jecha anaongoza Tume aliyoitusi isiaminike. Yuleyule aliyeisingizia kuvuruga uchaguzi, kwa jicho lake lenye makengeza, leo anatumika kuendesha uchaguzi wa marudio unaosaidia tu wakubwa fulani kuibia wananchi. Haieleweki.

error: Content is protected !!