September 23, 2021

Uhuru hauna Mipaka

January Makamba atwishwa zigo sekta ya nishati

Spread the love

 

WAZIRI wa Nishati, January Makamba, amepewa jukumu la kutatua changamoto za sekta ya nishati hasa umeme. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

January amekabidhiwa jukumu hilo leo Jumatatu, tarehe 13 Septemba 2021, baada ya kuapishwa kuwa Waziri wa Nishati, Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Mbali na January, mawaziri wengine walioapishwa leo ni, Dk. Stergomena Tax ( Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa). Dk. Ashatu Kijaji (Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari) na Makame Mbarawa (Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi).

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amewataka mawaziri hao akiwemo January wakatekeleze majukumu yao vizuri, huku akiwatahadharisha kwamba anahitaji uongozi wenye matokeo.

“Januari ukafanye vizuri, uteuzi wenu hauna maani ni wazuri kuliko walioko huko, kwangu mimi nataka kuona matokeo. Ukiona kuna haja ya kufanya marekebisho kwa yale uliyoyakuta tuandikie barua tutafanyia kazi,” amesema Rais Samia.

Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu wa Rais, Dk. Phillip Mpango, amemuagiza January akasimamie miradi mikubwa ya nishati hasa ya umeme inayotekelezwa na Serikali, ili isikwame.

“Makamba wewe sio mgeni katika baraza na katika sekta kama Spika Job Ndugai alivyosema. Kasimamie miradi yetu mikubwa isikwame unaifahamu vizuri, umeme vijijini ni kilio kweli kweli, nikuombe utupe jicho kali sana kwa watendaji wako wa Tanesco,” amesema Dk. Mpango na kuongeza:

“Nikusihi uangalie maeneo ya nchi yetu ambayo gridi ya umeme haijafika, hao nao ni Watanzania tusiwape nafasi ya kulalamika.”
Naye Spika Job Ndugai, amemtaka January akadhibiti uingiaji wa mikataba mibovu katika sekta zilizoko chini ya wizara yake, pamoja na kumaliza viporo vya madeni.

“ Ulipokuwa mwenyekiti wa Kamati ya Nishati ya Bunge ulifanya kazi vizuri, hivyo na hakika bado una kumbukumbu kubwa za sekta hii, wakati ule unashughulika mpaka sasa tulijikuta tuko kwenye madeni makubwa sana na mikataba ya ajabu sana ya eneo la nishati,” amesema Spika Ndugai.

Spika Ndugai amesema “tunatoka huku Serikali imejitahidi sana imeendelea kututoa huko tuwe na mikataba bora ya nishati hasa ya umeme.”

Spika Ndugai amemtaka January akakamilishe ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme wa Maji la Julius Nyerere, maarufu kama Stigler’s Gorge, ili kuondoa changamoto ya umeme nchini.

Job Ndugai

“Nishati ya umeme kuna wakati Kongwa umeme unakatika mara 30 kwa wakati mmoja au zaidi, ni kitu cha kawaida, lazima tutoke huko na jukumu hili ni la kwako pia, hatuwezi kuendelea bila ya nishati kwa hiyo maana yake Stigler Gorges inabidi imalizike kwa wakati wake,” amesema Spika Ndugai.

Kiongozi huyo wa Bunge amesema “eneo la gesi ni ambalo hapa katikati hatukulipa heshima yake na ni chanzo kikubwa cha utajiri, lazima eneo la gesi likafanyiwe kazi vizuri sana lipate heshima yake na nchi ipate mapato ya kutosha, ziko nchi zinaendeshwa kwa gesi peke yake na tunazifahamu.”

Hali kadhalika, Spika Ndugai, amemuagiza January akafufue mradi wa uunganishaji madini ya chuma na makaa ya mawe ya Liganga na Mchuchuma, mkoani Njombe.

“Mwisho katika eneo lako , ni Liganga na Mchumchuma, ni moyo wa uchumi wa nchi. Imezungumzwa sana huko nyuma, hebu tukazalishe umeme pale, tukatoe chuma iliyoko pale nchi hii iweze kutoka kiuchumi,” amesema Spika Ndugai.

Pia, Spika Ndugai amemtaka January akadhibiti mfumuko wa bei za mafuta hasa petrol na dizeli.

“Tuna tatizo kubwa la nishati ya petrol, dizeli na jamii zake zote, ni matarajio yetu utaingalia pia bei ya Petrol isipande kama inavyokwenda, tuangalie mbinu mbadala ya kufanya tukawa na stability kwenye eneo hilo,” amesema Spika Ndugai.

Wakati huo huo, Spika Ndugai amemtaka January akamalize tatizo la umeme kwenye maeneo ya vijijini.

error: Content is protected !!