January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Janjaweed wavamia, wamdhalilisha mwanamke

Moja ya matukio yaliyowahi kufanywa na Janjaweed kisiwani Zanzibar

Spread the love

MWANAMKE mmoja mwenye mume wakiishi kijiji cha Mtende, Wilaya ya Kusini Unguja, amedhalilishwa na wanaume watatu waliomvamia nyumbani kwake asubuhi leo kumshinikiza ahame Chama cha Wananchi (CUF) ili arudi CCM. Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Kwa sasa mwanamke huyo amelazwa kwenye hospitali binafsi ya Al Rahma akipatiwa matibabu ambako taarifa zinasema amechanganyikiwa akili.

Taarifa kutoka kijijini Mtende zimesema watu watatu walifika kiasi cha saa moja asubuhi leo na kuingia ndani kwa mwanamke huyo wakati mumewe akiwa ameshatoka kwenda shambani na kumtisha kwa kumtaka atamke mwenyewe kuhama CUF.

Mwandishi wa habari hizi amefahamishwa na viongozi wa mtaa wa Romlo kijiji Mtende kuwa watu hao walioficha nyuso zao walionekana wakati wanaingia ndani lakini hakuna aliyehofia kwa kudhani kuwa labda walikuwa wageni rasmi.

Hata hivyo hofu iliwapata walipobaini kuna vishindo na baadaye kilio kusikika na watu hao walipotoka walikuwa na hofu kubwa huku wakikimbia kwa kasi.

“Tulipokwenda kuangalia tulimkuta (wanamtaja kwa jina mwanamke aliyedhalilishwa) analia na kunung’unika. Alilalamika kuwa amedhalilishwa na watu waliomvamia na walimtishia kwa bastola alipokataa matakwa yao,” amesimulia kiongozi mmoja kijijini.

Kwa mujibu wa wato taarifa, mwanamke huyo aliulizwa maswali yaliyohusiana na sababu zilizomfanya kuhama CCM na kuhamia CUF na kama kuna mtu yeyote aliyemshawishi. Alikataa kujibu, imeelezwa.

Wananchi walimchukua mwanamke huyo na kuripoti tukio hilo kwa uongozi wa CUF Wilaya na kufanyika utaratibu wa kumpatia usafiri hadi hospitali ya Al Rahma, iliyopo Kilimani mjini Zanzibar.

Imani iliyopo kijijini Mtende ni kwamba waliokuja kufanya uhalifu huo ni askari wa vikosi vya SMZ wanaoitwa Janjaweed, ambao wamekuwa wakizusha fadhaa Zanzibar kwa kutumia silaha na kujeruhi wananchi wanaoona ni wafuasi wa CUF.

Makundi ya askari hao wa serikali walikuwa wakivamia vituo vya uandikishaji wapigakura na kusimamia mamluki waliotoka maeneo yasiyokuwa yao waandikishwe. Watu kadhaa wamejeruhiwa na gari za CUF kuchomwa moto.

Katika tukio mojawapo la vitendo vya askari hao, walimkamata msichana na kumbaka wanne mchana kweupe katika mwezi huu wa Ramadhan.

Viongozi wa jeshi la polisi wamepuuzia vitendo vya askari hao. Serikali pia imesema hakuna askari wa serikali wanaovamia na kupiga wananchi.

error: Content is protected !!