August 8, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Janja’ ya serikali yamkosesha dhamana Melo

Maxence Melo, Mkurugenzi Mtendaji wa mtandao wa Jamii Forums

Spread the love

MAXENCE Melo, Mkurugenzi Mtendaji wa mtandao wa Jamii Forums amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es salaam huku akishtakiwa kwa makosa matatu mbele ya mahakimu watatu tofauti, anaadika Faki Sosi.

Uamuzi wa serikali kumfikisha kortini Melo kwa makosa matatu yanayoshabihiana lakini kwa nyakati tofauti mbele ya mahakimu watatu tofauti umesababisha wadhamini wake kushindwa kumdhamini kwa wakati na hivyo kurejeshwa rumande – katika gereza la Keko.

Alianza kwa kushitakiwa katika kesi Na. 456 yenye shtaka moja alilosomewa mbele ya Thomas Simba, Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo ambapo alidaiwa kuzuia taarifa za upelelezi wa jeshi la Polisi.

Melo amedaiwa kuwa kati ya tarehe Mosi Aprili na tarehe 13 Desemba, 2016 huko Mikocheni, Kinondoni jijini Dar es Salaam Mkurugenzi huyo wa kampuni ya Jamii media inayoendesha mtandao wa Jamii forums alikataa kutoa taarifa za kiuchunguzi kwa Jeshi la Polisi zilizochapishwa kwenye mtandao huo.

Kesi nyingine ya pili imepewa Na. 457 ikiwa imesomwa mbele ya Hakimu Godfrey Mwambapa, ambapo Melo anadaiwa kati ya tarehe 10 Mei na tarehe 13 Desemba 2016 akiwa Mikocheni Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam alikwamisha kazi ya Jeshi la Polisi kwa kutotoa taarifa za kiupelelezi kwa jeshi la polisi.

Kesi ya tatu kwa Melo ni Na. 458 iliyosomwa mbele ya Hakimu Victoria Nongwa, ambapo wakili wa Serikali Mohammed Salim alidai kuwa Melo alikuwa anamiliki mtandao wa bila ya kusajiliwa hapa nchini Tanzania na kuwepewa msimbo wa (.co.tz), ikiwa ni kinyume cha sheria.

Anadaiwa kuwa kati ya tarehe 9 Desemba, 2011 mpaka tarehe 13 Desemba, 2016 akiwa kama Mkurugenzi wa Jamii media alikuwa anamiliki mtandao wa Jamii Forum bila kusajiliwa nchini Tanzania.

Mtuhumiwa alitimiza masharti ya dhamana katika kesi Na. 456 na 457 lakini katika kesi ya tatu ambayo ni Na. 458, alishindwa kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili baada ya wadhamini waliokuwepo kuwa wameshamdhamini katika kesi zingine hali iliyosababisha arudishwe rumande.

Kesi hiyo itatajwa tena Desemba 29 mwaka huu.

Akizungumzia hatua ya Melo kukosa dhamana katika kesi ya tatu Jebra Kambole, wakili wa upande wa utetezi amedai kuwa kilichowafanya wakose dhamana ni matakwa ya wadhamini katika kesi hizo ambapo walihitajika wadhamini wawili kwenye kesi namba 458 na mmoja kukosekana na kusababisha kurejeshwa rumande kwa mteja wake.

error: Content is protected !!