MUIMBAJI wa nyimbo za injili nchini Tanzania, Jane Misso amewaomba mashabiki zake kukaa mkao wa kula kwani sasa amenuia kurejea kwa kishindo baada kutosikika kwa muda mrefu. Anaripoti Rhoda Kanuti … (endelea).
Amesema amekuja kivingine kwa kuanza kutoa Remix ya wimbo wake wa ‘Omoyo’ alioutoa 2009 na sasa anamshirikisha Msanii wa Bongo fleva, Rajabu Abdul ‘Harmonize’.
Akizungumza na Mwanahalisi online hivi karibuni jijini Dar es salaam, mwimbaji huyo amesema kwa kipindi kirefu amekuwa akishughulika na majukumu ya familia.
Pia amesema mbali na uimbaji anajishughulisha na biashara ndogondogo yaani ujasiriamali.
Mama huyo wa watoto watatu amesema Harmonize alimuomba kufanya naye Remix ya wimbo huo wa Omoyo.
“Kwanza nilijiuliza kwa nini mimi! lakini nikajua Mungu anamakusudi yake,” amesema.
Hata hivyo, watu wamekuwa wakijiuliza, kwanini muimbaji wa nyimbo za injili, kumshirikisha muimbaji wa Bongo fleva.
“Niwaambie kwamba Mungu ni wetu sote. Nashukuru Mungu wimbo wangu umekuwa na muitikio mkubwa kutoka kwa mashabiki, hivyo hata wazo hili la kushirikiana na Harmonize naamini wengi wao wataupenda wimbo wetu.
“Hata Yesu alipomuona Zakayo aliyekuwa mtoza ushuru akamwambia… twende nyumbani kwako tukale pamoja, wafuasi walimshangaa Yesu kwakuwa Zakayo alikuwa mnyanganyi.
“Hivyo niwaombe shabiki zangu tuendelee kuombeana, nyimbo zipo nimeziandaa hivi karibuni zitatoka,” amesema.
Leave a comment