JAMII imesisitizwa kuona umuhimu wa utunzaji wa vyanzo vya maji utakaosaidia kutorudisha nyuma jitihada za upandaji miti na uhifadhi wa mazingira zinazofanywa nchini. Anaripoti Christina Haule, Morogoro … (endelea).
Ofisa Misitu mwandamizi kutoka Ofisi ya Bodi ya maji Bonde la Wami Ruvu kitengo cha kuhifadhi mazingira Emmanuel Komba alisema hayo jana wakati wakiadhimisha wiki ya maji huku wakipalilia miti 800 iliyopandwa mwishoni mwa mwaka jana pembezoni mwa Bwawa la Mindu Manispaa ya Morogoro.
Alisema wapo watu wanamilika mifugo na wanachungia kandokando ya Bwawa na kwenye miti iliyopandwa ambapo elimu zaidi wanaendelea kuitoa ili uwepo umuhimu wa kuyahifadhi maeneo hayo kwa manufaa ya wote.
Hivyo alisema mifugo ni vema ikatengewa maeneo tofauti na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kuhifadhi vyanzo vya maji ili kuvinusuru vyanzo hivyo.
Alisema maeneo vya vyanzo vya maji pia wananchi wamekuwa wakichoma moto hivyo ni jukumu la kila mwananchi kuyalinda kwa kuepuka moto sababu wao watapanda na miti itakua na kama mwananchi mwenye nia mbaya akichoma moto atakuwa amewarudisha nyuma.
Alisema vyanzo vya maji lazima vitunzwe na ni jukumu la kila mmoja sababu maji hayana mbadala kwa kila mmoja.
Maadhimisho ya Wiki ya maji duniani yameanza rasmi Machi 16 na yanatarajia kukamilika Machi 22 na kitaifa yanafanyika jijini Dar es Salaam huku yakiwa na kauli mbiu ya ‘kuongeza kasi ya mabadiliko katika sekta ya maji kwa maendeleo endelevu ya uchumi’
Leave a comment