December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Jamhuri wafunga ushahidi, kina Mbowe waanza kujitetea

Spread the love

 

UPANDE wa Jamhuri katika kesi ndogo ndani ya kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu, umefunga ushahidi katika kesi hiyo, kwa kuleta mahakamani mashahidi wanne kati ya sita uliyopanga kuwaita. Anaripoti Regina Mkonde, Dar ea Salaam … (endelea).

Kesi hiyo ndogo ni ya kupinga maelezo ya onyo ya mshtakiwa, Mohammed Abdillah Ling’wenya yasipokelewe mahakamani kama kilelezo wakidai hayakutolewa na mshtakiwa huyo bali alilazimishwa kusaini karatasi iliyodaiwa kuwa na maelezo yake.

Ushahidi huo umefungwa leo Alhamisi, tarehe 25 Novemba 2021 katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mawasiliano jijini Dar es Salaam, mbele ya Jaji Joachim Tiganga.

Baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando kuiomba mahakama hiyo ifunge ushahidi.

“Baada ya kuwa tumepitia ushahidi wa mashahidi ambao wameshatoa ushahidi, tumeamua baada ya shahidi yule wa nne kumaliza hatutatoa ushahidi mwingine zaidi, badala yake tunaomba kufunga ushahidi wetu katika hatua hii ya kesi ndogo ndani ya kesi kubwa,” amedai Wakili Kidando.

Kufuatia ombi hilo, Jaji Tiganga alifunga ushahidi wa upande wa mashtaka, na kuwaita upande wa utetezi kuanza kutoa ushahidi.

“Baada ya upande wa mashtaka kama ilivyowasilisha, mahakama inafunga kesi upande wa mashtaka katika kesi ndogo inayomhusu mshtakiwa namba tatu, sababu hiyo basi niwaite upande wa utetezi kuanza kutoa ushahidi,” amesema Jaji Tiganga.

Wakili wa mshtakiwa huyo Fredrick Kihwelo, amedai mahakamani hapo wako tayari kujitetea ambapo Ling’wenya anaanza kutoa ushahidi wake akiongozwa na Wakili Dickson Matata.

Mashahidi wa jamhuri katika kesi hiyo ndogo walikuwa ni, Inspekta Lugawa Issa Maulid, Kaimu Mkuu wa Kituo cha Polisi Tazara Pugu Road akitanguliwa na Askari Mpelelezi H4347 Goodluck, Askari Mpelelezi Ricardo Msemwa na Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Arumeru, mkoani Kilimanjaro, SP Jumanne Malangahe.

Mashahidi hao wa upande wa mashtaka waliieleza mahakama hiyo namna Ling’wenya na mwenzake Adam Kasekwa, walivyokamatwa maeneo ya Rau Madukani, Moshi mkoani Kilimanjaro, tarehe 5 Agosti 2020, kwa kosa la kula njama za kupanga vitendo vya kigaidi.

Pia, waliieleza mahakama hiyo namna na sababu za watuhumiwa hao kutolewa mkoani Kilimanjaro kuja kuhojiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, kisha kuhamishiwa Kituo cha Polisi Mbweni, mkoani humo.

Walidai, mhumiwa huyo hakuteswa na wala hakulazimishwa kusaini karatasi yenye maelezo ya onyo kama inavyodaiwa na mawakili wa utetezi, bali alitoa maelezo hayo kwa hiari yake.

Mbali na Mbowe, Ling’wenya, Kasekwa mwingine ni Halfani Bwire ambao kwa pamoja wanadaiwa kupanga mipango ya ugaidi katika maeneo mbalimbali nchini kwa kulipua vituo vya mafuta.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI TV, MwanaHALISI Online na mitandao yetu ya kijimaa kwa habari na taarifa mbalimbali

error: Content is protected !!