April 14, 2021

Uhuru hauna Mipaka

James Mbatia: Tusipofanya maridhiano, tutaliangamiza taifa

Spread the love

MWENYEKITI wa NCCR- Mageuzi, James Francis Mbatia (55), ameonya kuwa hakuna maendeleo yanayoweza kufikiwa nchini, ikiwa umoja wa kitaifa uliosisiwa na Mwalimu Julius Nyerere, utavurugwa na warithini wake. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Akizungumza kwenye mkutano mkuu wa chama chake, leo tarehe 27 Julai kwenye ukumbi wa Diamond Jublee, Mbatia amesema, ili taifa liwe na maendeleo, lazima serikali na wananchi wake waondokane na ubinafsi.

Amesema, “…imani zote zinatufundisha udugu, utu na umoja; sasa ni nani mwenye kiburi?  Yatubidi kujitafakari upya,  kujitambua na kujua misingi ya taifa yetu.”

Mbatia amesema, “taifa letu likiharibika, tukigombana kwa sababu ya misingi ya fikra binafsi, sote tutaumia hakuna atakayebaki iwe vyama mbadala, CCM (Chama Cha Mapinduzi) mtaumia.”

Ameongeza: “Tanzania ni yetu sote hakuna mwenye hati miliki ya kuwatawala Watanzania milele, na tujifikirie utaifa wetu kwanza. Yote haya yatawezekana ikiwa tuna umoja wa kitaifa na wa kusikilizana, yote yatawezekana.”

Akizungumzia uchumi, Mbatia amesema hatua ya walioko serikalini kutosikiliza mawazo ya wengine, inarejesha nyuma maendeleo ya taifa.

Amesema, “serikali haitaki kusikiliza mawazo ya wengine, kwamba  bila kushirikisha sekta binafsi, uchumi wa nchi hauwezi kukukua.”

Amesema, “…huu ndio ukweli.  Sekta binafsi ndio injini ya uchumi.

Serikali waangalie namna ya kufanya maamuzi kwenye masuala ya kodi na kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji ambayo hayaleti vizingiti. Hiyo itasaidia wawekezaji kuwekeza nchini. Lakini nje ya hilo, hatutafika kokote.”

Amesema, sekta binafsi imeyumba kutokana na mazingira ya uwekezaji kutotabirika ikiwemo mabadiliko ya kila mara ya viwango vya kodi, hali inayoogopesha wawekezaji kuwekeza nchini.

Mbatia ametaja jambo jingine linalorudisha nyuma maendeleo ni kutokuwepo kwa uchumi unaoakisi soko, huku akiangazia kuvurugika kwa mchakato wa uuzaji wa zao la korosho katika msimu uliopita, na kusababisha nchi kukosa fedha za kigeni.

“Ni vyema zile kasoro ziondolewe na kujenga uchumi unaoakisi soko. Mfano uchumi wa korosho zao ambalo linaloongoza kuleta mapato ya kigeni kuliko mazao yoyote,” ameeleza.

Mkutano mkuu wa NCCR- Mageuzi, pamoja na mengine, unatarajia kuchagua viongozi wapya wa chama hicho watakaoongoza kwa miaka mitano ijayo.

error: Content is protected !!