January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

James Mbatia: Hatuondoki UKAWA

Spread the love

CHAMA cha NCCR-Mageuzi kimesema hakuna namna kinaweza kujitenga na ushirikiano na vyama vitatu vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA). Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia amesema “Mimi na chama changu hatuwezi kuondoka Ukawa.” Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Mbatia ambaye kitaaluma ni mhandisi, ametoa msimamo huo leo katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya chama, Ilala, jijini Dar es Salaam.

Amesema taarifa yoyote itakayotolewa kuhusu kujitoa lazima itangazwe na yeye mwenyekiti ambaye kwa mujibu wa katiba ya chama hicho ndiye msemaji wa chama.

“NCCR-Mageuzi ni mtoto wa Ukawa. Ukawa ni sauti ya wananchi. Ukawa sio vyama vya siasa. Ukawa ni wananchi. Wanasiasa ndani ya Ukawa wataondoka lakini Ukawa utabaki palepale. Hivyo ninawahakikisha NCCR haijafanya uamuzi wala haina nia ya kuondoka UKAWA,” alisema.

Mbatia amekuwa mwenyekiti mwenza tangu UKAWA ulipoanzishwa kabla ya kumalizika kwa awamu ya kwanza ya mkutano wa Bunge Maalum la Katiba mwaka 2013, lilipokuwa limejadili Sura mbili tu za Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Wajumbe wa bunge hilo kutoka vyama vya UKAWA walisusia mkutano na kutoka nje na kurejea majimboni kwao. Uamuzi wao ulikuja baada ya kujiridhisha kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimedhibiti sehemu kubwa ya wajumbe wa bunge na kufanikiwa kuvuruga rasimu hiyo kwa kuondoa msingi au moyo wa rasimu yenyewe uliopendekeza, pamoja na mambo mengine, katiba ya mfumo wa serikali tatu badala ya mbili.

Msimamo wa msisitizo alioutoa Mbatia wa kujiimarisha ndani ya UKAWA umetokana na taarifa zilizochapishwa na toleo la leo la gazeti la UHURU, linalomilikiwa na kuchapishwa na CCM kwamba NCCR-Mageuzi imejiondoa UKAWA.

Gazeti hilo limechapisha taarifa hizo kwa kuzungumza na Faustine Sungura, Afisa katika Idara ya Kampeni na Uchaguzi ya chama hicho.

error: Content is protected !!