August 8, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Jambazi ‘kinda’ afunga mtaa

Spread the love

MTOTO anayesadikiwa kuwa na umri kati ya miaka 15-17 amefunga Mtaa wa Mecco, Kata ya Nyakato wilayani Nyamagana, Mwanza kwa kupiga risasi hewani na kusababisha taharuki kubwa kwa wafanyabiashara na Wananchi, anaandika Moses Mseti.

Tukio la kijana huyo ‘kufunga mtaa’ limetokea usiku wa jana saa 1:45 katika Mtaa wa Mecco stendi, baada ya (kijana) huyo kutaka kupora katika duka moja linalouza mtungi ya gesi na vifaa vingine.

Inaelezwa kuwa, kijana huyo baada ya kufika katika duka hilo kama kama, baada ya muda mfupi mfanyakazi wa duka hilo (jina halijafahamika)  alimshutukia na kuanza kupambana naye.

Hata hivyo, katika mapambano ya wawili hao, kijana huyo alianza kupiga kelele zilizosikika, ‘niachieni, niachie’ huku mfannyakazi wa duka hilo akiomba omba msaada kwa watu waliokuwa karibu na duka hilo.

Baada ya watu kufika huku mfanyakazi wa duka hilo, akiita ‘mwizi mwizi,’ watu walifika na kumshika kijana huyo.

Kijana huyo aliwaponyoka na kutoa silaha iliyokuwa kwenye begi na kupiga risasi moja hewani kuwatawanya watu waliokuwa eneo hilo.

Pia baada ya kijana huyo kupiga risasi hiyo, gari ndogo nyeupe ilifika na kumchukua na kutokomea kusikojulikana, kitendo hicho kilisababisha wananchi wa eneo hilo kupigwa butwaa.

Daud Machota, mmoja wa Wananchi wa eneo hilo amesema kuwa, vitendo vya uhalifu katika eneo hilo vimeanza kutishia amani kwani kumesababisha watu wengi kulala mapema.

“Kwanza mimi ninachoshangaa inakuaje mtoto mdogo wa miaka 15 – 17 anashika silaha na kupiga risasi hewani, labda hawa watoto wanaweza wakawa wamefunzwa mafunzo ya kigaidi, haiwezekani kwa umri wake kufanya hivyo,” amesema Machota.

Machota amesema kuwa, kijana huyo alifanikiwa kuchukua kiasi cha Sh. 40, 000  kwenye duka hilo, huku akidai kwamba uhalifu huo unasababishwa na ugumu wa maisha unaonekana kuwagusa watu wengi.

Ahmed Msangi, Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza na Naibu Kamishna wa Polisi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akidai kuwa, askari walikuta katika eneo la tukio begi na shati moja.

“Hakuna mtu aliyejeruhiwa katika uhalifu huo, tunaendelea na uchunguzi kuwakamata watu wanaofanya vitendo hivyo, ilipigwa risasi moja hewani,” amesema Msangi.

Vitendo vya uhalifu wa kutumia silaha za moto katika kipindi cha hivi karibuni, vimeshamiri jijini humo na kusababisha wananchi na wafanyabiashara wa maduka, kuishi kwa hofu.

Tarehe 31 Novemba mwaka huu matukio mawili ya uhalifu wa kutumia silaha za moto yalifanyika kwa wakati tofauti na kusababisha watu wawili kujeruhiwa na kuporwa fedha kiasi cha Sh. 1.2 Milioni katika Mgahawa wa The Dinners.

Kashamiri kwa matukio hayo kumesababisha baadhi ya watu jijini humo kulaumu vyombo vya usalama kwa kushindwa kudhibiti hali hiyo.

error: Content is protected !!