Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Jaji Warioba akosoa viongozi kuingilia mikutano ya Rais Samia
Habari za SiasaTangulizi

Jaji Warioba akosoa viongozi kuingilia mikutano ya Rais Samia

Jaji,Joseph Warioba Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
Spread the love

 

JOSEPH Sinde Warioba, Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania, amewataka viongozi kujenga utamaduni wa kusikiliza kero za wananchi wanapokwenda kwenye mikutano mbalimbali. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

Jaji Warioba aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, amesema hayo hivi karibuni katika mahojiano maalum katika kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na televisheni ya ITV.

Katika mahojiano hayo, Jaji Warioba amezungumzia masuala mbalimbali ikiwemo utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan, mchakato wa katiba mpya, utawala bora na nasaha zake kwa viongozi.

Jaji Warioba amegusia utaratibu wa Rais Samia kukutana na makundi mbalimbali unapaswa kuendelea huku akikosoa utitiri wa viongozi kwenye mikutano hiyo.

Tangu Rais Samia aingie madarakani, tarehe 19 Machi 2021, baada ya kifo cha aliyekuwa Rais John Magufuli, amekutana na makundi mbalimbali ikiwemo wazee wa Dar es Salaam, wanawake mkoa wa Dodoma, Vijana Mkoa wa Mwanza na sekta binafsi.

Makundi mengine ni; wahariri na waandishi wa habari, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Jumuiya ya Kikristu Tanzania (CCM).

Jaji Warioba alisema “mimi naona hili ni jambo zuri, lakini hii inapaswa kulenga watu anaokutana nao, nimeona alipokutana na vijana, viongozi walikuwa wengi karibu saa tatu wanaongea wao.”

“Kama Rais anakutana iwe ya Rais, mawaziri na viongiozi wengine wana nafasi zao nyingi tu za kuongea nje ya mikutano hiyo. Lakini anapokutana na makundi hayo ni vizuri kuwasikiliza wao wenyewe, inaonekana viongozi ndio wanazungumza kero zao,” alisema

Jaji Warioba aliyekuwa waziri mkuu kati ya mwaka 1985 hadi 1990 alisema, “afanye kama alivyofanya kwenye sekta binafsi na wanahabari. Si viongozi kwenda kusema matatizo ya wananchi, nafikiri wasaidizi wake wataweka utaratibu mzuri zaidi.”

Rais Samia Suluhu Hassan

Alitolea mfano, akiwa waziri mku, alifanya ziara katika Kijiji kimoja mkoani Arusha ambapo alikaribishwa kwa shangwe zilizoambatana na ngoma.

Alisema, katika mkutano ule, walizungumza viongozi mbalimbali ikiwemo kusoma risala iliyokuwa imeandaliwa, “kisha nikakaribishwa, mimi nikasema muda bado upo wacha tusikilize wananchi wanasema nini.”

“Mwananchi mmoja akasema, mheshimiwa waziri mkuu, umesikiliza risala ya viongozi, sasa sikiliza risala yetu ya wananchi na kile walichokisema ni tofauti kabisa na ile ya viongozi,” alisema

Jaji Warioba alisema, “niliporudi Dodoma, kulikuwa na kikao fulani hivi na Mwalimu Nyerere, nikamweleza nina mashaka kama hiki tunachokifanya ndicho wananchi wanataka.”

Alisema, Mwalimu Nyerere alimweleza ili uwe unapata ukweli wa mambo, anapopanda gari aangalie wananchi walivyo, hali ya barabara, akifika mkutanoni jinsi anavyopokelewa, nyimbo zinazoimbwa na mashairi yatakuwa na ujumbe ambao utamsaidia kubaini baadhi ya mambo.

“Ukifanya haya yote utaelewa matatizo ya nchi, matatizo ya wananchi na hivyo utajifunza kitu na ukiwasikiliza utakuwa utabaini kitu. Ninataka kusema, viongozi tuwe na utaratibu wa kuwasikiliza wananchi na si kuwahutubia tu, ni muhimu sana kujifunza kutoka kwa wananchi,” alisema

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!