October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Jaji mstaafu Othuman Chande apewa shavu ICC

Spread the love

ALIYEKUWA Jaji Mkuu wa Tanzania, Othuman Chande, ameteuliwa na Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, inayojihusisha na uhalifu dhidi ya wanadamu na uhalifu wa kivita (ICC), Karim Asad Ahmad Khan, kuwa mmoja wa washauri wake maalum. Anaripoti Mwanaharusi Abdallah, TUDARCo…(endelea)

Taarifa kutoka makao makuu ya ICC, jijini The Hague nchini Uholanzi zinasema, Jaji mstaafu Chande, ni miongoni mwa wataalamu 17 walioteuliwa na kiongozi huyo wa mashitaka.

Uteuzi wa washauri hao wa Khan, umezingatia maeneo wanayo, jinsia pamoja na utaalamu wao wa masuala mbalimbali hususan ya kisheria.

Chande alihudumu nafasi ya Jaji Mkuu wa Tanzania kuanzia tarehe 28 Desemba 2010, baada ya kuteuliwa na Rais wa wakati huo, Jakaya Mrisho Kikwete, akichukua nafasi ya Augustino Ramadhan ambaye alistaafu kwa mujibu wa sharia. Kwa sasa Jaji Ramadhani ni marehemu.

Jaji Chadema aliongoza muhimili huo wa Mahakama hadi tarehe 28 Januari 2017 alipostaafu na Rais wa wakati huo, John Pombe Magufuli alipomteua Profesa Ibrahimu Juma kuvaa viatu vyake. Kwa sasa Magufuli ni marehemu.

Mahakama ya ICC, inatumika kushitaki kwa makosa ya uhalifu ikiwamo mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu mwingine, ilianzishwa ili kuisaidia kazi mifumo ya kitaifa ya mahakama za nchi tofauti.

Aidha, mahakama hiyo, inakuwa na mamlaka pale mahakama za kitaifa zinapokataa ama zinaposhindwa kufanya uchunguzi ama kuendesha mashitaka juu ya uhalifu wa aina hii.

Kwa mujibu wa rekodi zilizopo, takribani nchi 120, ni wanachama wa mahakama ya ICC, huku nchi nyingine zaidi ya 30 ikiwamo Urusi zimejiandikisha lakini bado hazijaridhia mkataba wake.

Kwa sasa, Jaji Othuman Chande, ni mmoja wa watu wanaounda jopo la watalaamu wa Umoja wa Mataifa (UN), wanaochunguza kifo cha aliyekuwa katibu mkuu wa pili wa umoja huo, Dag Hammarskjold.

Mahakama ya ICC, iliundwa miaka 23 iliyopita, kupitia mkataba wa Roma wa 17 Julai 1998.

Tangu kuundwa kwake, ICC imechunguza kesi zaidi ya 32, nyingi zikiwa bado katika awamu ya majaribio, imetoa waranti 35 za kukamatwa, 17 zilitekelezwa huku ikiwa na wafungwa nane ambao wote wanazuiliwa.

Ilichukua miaka 14 baada ya kupitishwa kwa Sheria ya Roma ili kuona mtuhumiwa wa kwanza wa ICC aakihukumiwa.

Thomas Lubanga, kiongozi wa wanamgambo wa Ituri ambaye alihukumiwa miaka 14 jela mwaka 2012, baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kuajiri watoto jeshini, ni miongoni mwa vigogo waliohukumiwa na mahakama hiyo.

Kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa Lubanga, kuliwapa wasiwasi viongozi wa makundi ya waasi.

Hata hivyo, mahakama hiyo imeendelea kukosolewa na wataalamu wa maswala ya sheria ambao wanaona kuwa kuna makosa mengi ambayo yanafanyika lakini ICC imeshindwa kuyashiguhulikia.

Kwa hatuwa ya kwanza mahakama ya ICC ilianza kuchunguza makosa yanayotendeka barani Afrika ambapo awali ni mataifa yenyewe ya Afrika ndio yalitowa wito kwa ICC kuchunguza makosa.

Wakati mahakama hiyo ilianza kuwashambulia viongozi kama vile Omar el Bachir wa Sudani, Uhuri Kenyatta wa kenya na naibu wake William Rutto, Umoja wa Afrika ulianza kulalama kuwa mahakama hiyo sasa yaonekana kuwa ni ya wazungu dhidi ya wa Afrika.

Naye kiongozi wa zamani wa waasi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), John Bosco Ntaganda, alitiwa hatiani na mahakama hiyo, kwa makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binaadamu aliyoyatenda nchini mwake.

Bosco Ntaganda, aliyejulikana kwa jina la ”Terminator,” alipatikana na hatia ya makosa 18 ya uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya binadamu ikiwemo makosa ya mauaji, ubakaji na kuwasajili watoto jeshini yaliyotekelezwa Ituri nchini DRC kati ya mwaka 2002 hadi 2003.

Majaji walisema, Ntaganda, mwenye umri wa miaka 45, ”kiongozi mkuu wa waasi” alikuwa akitoa amri kuwalenga na kuwaua raia.”

error: Content is protected !!