Saturday , 25 March 2023
Home Gazeti Habari Mchanganyiko Jaji Mkuu Tanzania atoa mwelekeo matumizi ya Kiswahili mahakamani
Habari Mchanganyiko

Jaji Mkuu Tanzania atoa mwelekeo matumizi ya Kiswahili mahakamani

Spread the love

JAJI Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma, ameagiza mahakimu na majaji kuanza kutoa muhtasari wa hukumu kwa lugha ya Kiswahili, kuanzia Februari 2021. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Prof. Juma ametoa agizo hilo leo Jumatatu tarehe 18 Januari 2021, jijini Dar es Salaam, wakati anaelezea utekelezwaji wa agizo la Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Mwigulu Nchemba, la sheria kutafsiriwa kwa Kiswahili.

“Kila hukumu itakayosomwa kuanzia mwezi wa pili, mfano jaji akitoa hukumu, anatakiwa atayarishe muhtasari kwa lugha ya Kiswahili ambayo inaelimisha zaidi,” amesema Prof. Juma.

Tarehe 22 Desemba 2020, Dk. Mwigulu aliiagiza wizara yake kuzifanyia marekebisho sheria na sera, ili sheria zilizopo na zitakazotungwa, zitumie lugha ya Kiswahili.

Huku akihimiza taasisi zilizo chini ya wizara hiyo, zianze kutumia lugha ya Kiswahili katika kuhudumia wananchi.

Akizungumzia utekelezaji wa agizo hilo, Prof. Juma amesema, kila hukumu itaambatana na muhtasari wa Kiswahili.

“Kwa hiyo, ni vizuri tutafute namna gani kusaidia wananchi, lakini sisi kwa kuanza tutatumia Kiswahili katika muhtasari. Kila hukumu inapotoka itaambatana na muhtasari wa Kiswahili ambayo itaelimisha na kusaidia mwannanchi kukata rufaa anayohitaji,” amesema Prof. Juma.

Prof. Juma amesema, ili mahakama ianze kutumia lugha ya Kiswahili katika shughuli zake zote, inahitaji matayarisho, ikiwemo marekebisho ya sheria zilizopo, ili ziruhusu sheria zitafsiriwe kutoka lugha ya kingereza na kuwa Kiswahili.

“Tulikubaliana suala la kwanza itakuwa Serikalini, wabadilishe sheria, watafsiri sheria zote ambao ni muhimu zinatumika. Na sheria zikibadilika ina kuwa ni rahisi sana kwa mahakama kuweza kutumia neno la Kiswahili,” amesema Prof. Juma.

Vilevile, Prof. Juma amesema, mhimili huo uko katika taratibu za kutumia mifumo ya kidigitali ambayo inatafsiri lugha.

“Katika karne ya 21 ukisoma kwenye majarida, wenzetu China wameweza kabisa kuweka mifumo ambayo inafanya tafisiri papo kwa papo, hii ni karne ya 21 ni ya mapinduzi ya viwanda,” amesema.

“Wenzetu wametumia hayo mapinduzi kuweza kubadilisha, kunakuwa na programu ambayo ninapozungumza hapa unaweza kupata tafsiri papo kwa papo lugha yoyote ile,” amesema Prof. Juma.

Prof. Juma amesema “Ni jambo linalohitaji matayarisho na sisi tumeanza na hatua ya kwanza tutakayochukua ni kuangalia hizo software. Na vilevile kila hukumu ambayo itakayosomwa kuanzia mwezi wa pili jaji akitoa hukumu, anatakiwa atayarishe muhtasari kwa lugha ya Kiswahili.”

Kiongozi huyo wa Mahakama nchini Tanzania amesema njia hiyo itasaidia kuokoa muda wa mahakimu katika uandaaji wa hukumu.

“Sasa huko ndio tunatakiwa kwenda kwa sababu hatutaki hakimu badala ya kuzalisha hukumu 100, azalishe hukumu 20 sababu muda mwingi anapoteza kwenye kutafsiri. Wananchi watarudi na kulalamika,” amesema Prof. Juma.

Hata hivyo, Prof. Juma amesema lugha ya Kiswahili imeanza kutumika katika mahakama za mwanzo.

“Katika ngazi za mahakama ya mwanzo shughuli zote zinafanyika katika lugha ya Kiswahili, mahakama za mwanzo zinasikiliza kesi kwa asilimia 70 kwenye mashauri yote, tunaweza kusema kiswahili tayari kinatumika kwa asilimia 70,” amesema Prof. Juma.

Kuhusu Mahakama za Wilaya, Hakimu Mkazi, Mahakama Kuu na Rufani, Prof. Juma amesema, shughuli zake bado zinafanywa kwa kutumia lugha ya Kingereza, isipokuwa kama mawakili hawapo kinatumika Kiswahili.

“Katika Mahakama za Wilaya, Hakimu Mkazi, Mahakama Kuu na Rufani bado kumbukumbu za mahakama zina andikwa katika lugha ya Kingereza, lakini shughuli za mahakama kama hakuna mawakili mara nyingi mazungumzo yanakuwa kwa Kiswahili,” amesema Prof. Juma.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Watendaji Kata, Mitaa watakaoshindwa kusimamia usafi kukiona

Spread the love  WATENDAJI wa kata, mitaa na vitongoji na maofisa afya...

Habari Mchanganyiko

Mtia nia urais TLS kukata rufaa kupinga kuenguliwa

Spread the love  MTIA nia ya kugombea Urais wa Chama cha Mawakili...

Habari Mchanganyiko

NBC yazindua kampeni ya mkeka wa ushindi na ATM zake

Spread the loveBENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imetangaza uzinduzi wa kampeni...

Habari Mchanganyiko

Uholanzi wampongeza Rais Samia kuimarisha vyombo vya habari, demokrasia

Spread the love  UBALOZI wa Uholanzi nchini Tanzania, umempongeza Rais Samia Suluhu...

error: Content is protected !!