JAJI Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, amevunja ukimya kuhusu taratibu za uteuzi wa Majaji wa Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu wanavyopatikana. Anaripoti Mwandishi Wetu., Dar es Salaam … (endelea).
Amesema hayo leo Jumatatu, tarehe 17 Mei 2021, Ikulu ya Dar es Salaam, mara baada ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kumaliza kuwaapisha majaji saba wa Mahakama ya Rufani na 21 wa Mahakama Kuu.
“Vigezo vilivyotumika na kamati ndogo ya Tume ya Utumishi wa Mahakama kupata majina, ilizingatia uadilifu, wale waliokuwa na changamoto ya kimaaidli waliachwa ,” amesema Prof. Juma.
Ametaja vigezo vingine ni ” uzoefu wakutosha katika kazi za kisheria au mahakama, muda uliobaki kabla ya kustaafu, uwezo wa kujieleza, uelewa wa namna mahakama zinavyofanya kazi na baada ya uchambuzi kamati ilibaki majina 84, ambayo yaliwasilishwa kwa Rais.”
Ufafanuzi wa taratibu hizo umetolewa na Prof. Juma, baada ya baadhi ya watu kukosoa uteuzi wa Biswalo Mganga, kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Watu hao walidai kuwa, Mganga wakati akiwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), alitumia vibaya mamlaka yake.
Akielezea utaratibu huo, Prof. Juma amesema “kwa ufupi nielezee utaratibu uliotumika hadi Tume ya Utumishi wa Mahakama kuwasilisha mapendekezo kwako, kwa mujibu wa Ibara 113 Ibara ndogo 1 ya katiba ikisomwa na kifungu 29 cha Sheria ya Uendeshaji mahakama.”
“Tume imepewa jukumu kukushauri kuhusu uteuzi wa majaji wa mahakama kuu ili kuwapata majaji wa mahakama kuu uliyowapaisha leo.”
“Septemba 2020, tume ilimuelekeza mwenyekiti wake ambaye jaji mkuu, awaombe rasmi wadau mbalimbali wa sekta ya sheria kuwasilisha majina ya Watanzania wenye sifa za kikatiba, kuteuliwa kuwa majaji,” amesema Prof. Juma.
Amesema baada ya wito huo, wadau mbalimbali waliwasilisha katika tume hiyo, majina ya watu wlaiopendekezwa kupata teuzi hizo.
“Wadau wa sekta ya sheria waliwasilisha tume majina 232, 141 wanaumena 91 wanawake, mchanganuo wa majina walitoka kwa wadau wafuatao, kutoka mahakama walileta majina 87, mawakili wa serikali 30, wizara na taasisi za umma 36, vyuo vikuu 22, wakili wa kujitegemea walileta majina 53,” amesema Prof. Juma.
Pia, Prof. Juma amesema, mabaraza ya ardhi yaliwasilisha majina manne huku njia nyingine zilizotumika kupata majaji hao, ilikuwa kanzi data ya Mahakama, kupitia orodha ya maafisa wa mahakama waandamizi.
“Kupitia kamati ndogo ya tume, ilipitia majina na iliyachambua na kulinganisha sifa ya kikatiba ambapo tuliweza kupata majina yaliyofanyiwa usaili,” amesema Profesa Juma
“Kamati iliwasisha majina 46 kwa tume kwa ajili ya kujadiliwa, hakuna hata mmoja wetu aliyeomba nafasi ya ujaji lakini mlipendekezwa,” amesema Prof. Juma.
Kiongozi huyo wa Mahakama amesema baada ya mchujo huo, yalibaki majina 84 kati 232, ambayo yaliwasilishwa kwa Rais Samia, kwa ajili ya uteuzi.
Leave a comment