May 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Jaji Mkuu, Spika Ndugai wataka DPP, Takukuru watende haki

Job Ndugai, Spika wa Bunge la Tanzania

Spread the love

 

JAJI Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma, amemshauri Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Sylvester Mwakitalu, aanze majukumu yake mapya kwa kuyapatia ufumbuzi malalamiko ya wananchi, kuhusu ofisi yake. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Pia, Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuacha “kuonea watu kwa kwani haipendezi hata kidogo.”

Prof. Juma ametoa ushauri huo leo Jumatano tarehe 19 Mei 2021, baada ya DPP Mwakitalu kuapishwa na Rais Samia kushika wadhifa huo, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Mwakitalu, amechukua nafasi ya Biswalo Mganga ambaye yeye ameapishwa juzi Jumatatu, kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

“Katika maslahi ya umma DPP, lazima asikilize watu wanasema nini, watu wanalalamika wapi na wapi kuna tatizo. Hayo ndiyo maeneo ya kwanza yenye kuangalia,” amesema Prof. Juma.

Pia, Prof. Juma amemshauri DPP Mwakitalu atembelee tovuti za Mahakama ili aone mrundikano wa kesi uliopo, kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto hiyo.

“Sisi kwetu mahakamani tunamkaribisha atembelee tovuti za mahakama, tunaweka takwimu maeneo gani ambayo kuna ucheleweshaji sana. Sababu tumejiwekea utaratibu kesi zikifikia muda fulani katika mtandao wetu inaonesha alama nyekundu,” amesema Prof. Juma.

Kiongozi huyo wa mhimili wa Mahakama, amesema “tunaomba atembelee mfumo wa mahakamani waweze kuangalia wapi kuna changamoto ya ucheleweshaji.”

Prof. Juma amesema katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam kuna kesi 310 zimecheleweshwa.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma

“Na leo nimetembelea Mahakama ya Kisutu katika kesi zilizocheleweshwa kuna kesi 310, ambazo zimevuka muda ambao mahakamani zinaingia katika eneo la mrundikano. Tafuteni hizo taarifa ili mjipange kubadilisha,” amesema Prof. Juma.

Aidha, Prof. Juma amemtaka DPP Mwakitalu pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), Kamishna wa Polisi, Salum Hamduni, waweke wazi sheria zinazokwamisha utendaji wa majukumu yao, ili zifanyiwe marekebisho.

Hamduni, aliyekuwa Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Arusha, ameapishwa leo Jumatano, kuchukua nafasi ya Brigedia Jenerali John Mbungo ambaye atapangiwa kazi nyingine.

“DPP na mkurugenzi mkuu Takukuru, mnavaa viatu vya utendaji haki, kama kuna upungufu katika sheria na taratibu ninyi ndiyo mstari wa mbele kutuambia hatuwezi jua tatizo liko wapi,” amesema Prof. Juma na kuongeza:

“Msione haya kubadili sheria sababu zimetungwa kwenye zama za zamani kidogo na tuko kwenye zama ambazo wananchi wanataka kesi zizendeshwe kwa haraka kidogo.”

Rais Samia Suluhu Hassan

Naye Spika wa Bunge, Job Ndugai amemshauri DPP Mwakitalu akaimarishe ofisi yake, huku akimshauri Hamduni kuhakikisha anaondoa changamoto ya baadhi ya wananchi kuonewa na maafisa wa taasisi hiyo.

“Kumekuwa na maonezi makubwa sana Takukuru, si vizuri kuonea watu, haipendezi hata kidogo. Mkajiangalie upya sisi tunaowakilisha wananchi tunaona. Hapa si mahali pa kusema lakini Waziri Mchengerwa atawaambia,” amesema Spika Ndugai.

Spika Ndugai amesema, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa, atawafikishiwa ujumbe Takukuru wa maeneo wanayopaswa kuyafanyia kazi.

error: Content is protected !!