WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Ashatu Kijaji, amepewa kibarua cha kuziunganisha taasisi za Serikali na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA). Anaripoti Patricia Kighono, TUDARCo … (endelea).
Dk. Ashatu amekabidhiwa jukumu hilo leo Jumatatu, tarehe 13 Septemba 2021 na Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma, pamoja na Spika wa Bunge, Job Ndugai, baada ya kuapishwa kuiongoza wizara hiyo, Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.
Dk. Kijaji ameapishwa siku moja baada ya kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kuongoza wizara hiyo, akichukua mikoba ya Dk. Fuastine Ndugulile ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Prof. Juma, amemuomba Dk. Kijaji, aziunganishe mahakama katika mkongo wa taifa wa mawasiliano, ili ziende sambamba na mabadiliko ya TEHAMA.
“Pongezi nitoe kwa waziri wa TEHAMA ambayo sisi mahakama yangu namtegemea sana kutusaidia kuingia katika karne ya 21, ambayo rais umewahi kusema inasukumwa na mapinduzi ya nne ya viwanda. Tunategemea mkongo wa Taifa utaendelea kuunganishwa na mahakama zetu,” amesema Prof. Juma.
Aidha, Prof. Juma amemuomba Dk. Kijaji ashushe gharama za vifurushi vya intaneti, ili kurahisisha matumizi ya TEHAMA nchini.
“Gharama za internet zitashuka sababu hiyo ndiyo barabara iliyobaki kufikia mapinduzi ya nne ya viwanda,” amesema Prof. Juma.
Naye Spika Ndugai amemuomba Dk. Kijaji aziunganishe taasisi za Serikali na mifumo ya TEHAMA, ili kupunguza gharama zinazotumika katika kuchapisha ripoti na taarifa mbalimbali, ikiwemo za mabaraza ya madiwani.
“Kwenye teknolojia ya habari dunia ya sasa iko kwako, utusaidie sana kama alivyosema Jaji Mkuu, mabadiliko ya teknolojia ni muhimu katika maendeleo ya wananchi na hasa katika kupunguza gharama za Serikali,” amesema Spika Ndugai na kuongeza:
“Yako maeneo ya improvement mengi, ukitazama vile mabaraza ya madiwani yaliyotapakaa nchi nzima yanavyotumia makabrasha ya karatasi, tukiingia kwenye TEHAMA tutapunguza gharama kwa kiasi kikubwa sana, lakini hata vikao vya madiwani vitapungua,”
“Na katika maeneo mbalimbali ya utumishi na utoaji huduma, inakuwa bora zaidi kupunguza rushwa sababu mteja na mtoa huduma hawakutani uso kwa uso.”
Leave a comment