August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Jaji Mkuu awataka mahakimu wajitenge na siasa

Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma

Spread the love

 

JAJI Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, amewataka mahakimu wasijihusishe na masuala ya siasa, kwani yamepigwa marufuku na Ibara ya 113 A ya Katiba ya nchi. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Prof. Juma ametoa wito huo leo Jumamosi, tarehe 16 Julai 2022, akiwaapisha mahakimu wakazi wapya 20, jijini Dar es Salaam.

“Naomba msome Ibara ya 113 A , ya katiba ambayo inasema itakuwa ni marufuku kwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji wa Mahakama Kuu, Msajili wa Mahakama ngazi yoyote, hakimu wa ngazi yoyote kujiunga na chama chochote cha siasa, isipokuwa utabaki na haki ya kupiga kura. Hivyo lazima tuelewane,” amesema Prof. Juma.

Kiongozi huyo wa mahakama, amewataka watendaji wa mhimili huo wasifanye vitendo au kutoa kauli ambazo zinahusiana na masuala ya siasa.

“Usifanye mambo au kutoa kauli ambayo mwananchi anaweza kukuhusisha na chama chochote, sababu sio lazima uwe mwanachama inaweza kuwa vitendo vyako, maneno unayosema, nguo unazovaa zikahusishwa, kwa hiyo yote ni vizuri tujiadhari sana,” amesema Prof. Ibrahim.

Katika hatua nyingine, Prof. Juma amewataka mahakimu kutoahirisha kiholela tarehe za utoaji hukumu au uamuzi.

“Jambo lingine ambalo mahakimu wamekuwa wakilifanya ambalo wananchi wamekuwa wakilalamika, ni kupanga tarehe ya kusoma hukumu halafu inafika husomi. Unapanga tarehe nyingine, inafika husomi. Wananchi wanakuwa na haki ya kukushuku,” amesema Prof. Juma.

error: Content is protected !!