January 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Jaji Mkuu ataka mawakili wajiongeze, waache kulalamika

Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma

Spread the love

 

JAJI Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma, amewashauri mawakili na wanasheria, watafute nafasi za kujiajiri wenyewe, badala ya kulalamika kuna uhaba wa nafasi za ajira. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza wakati anawaapisha mawakili wapya, kwenye Viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam, leo tarehe 9 Julai 2021, Prof. Juma amewataka wajiongeze katika kupata ujuzi wa ziada, ili wakidhi matakwa ya soko la ajira lililopo sasa.

“Karne ya 21 inazo ujuzi, umahiri na sifa ambazo kwa bahati mbaya hatuzipati, katika vyuo na maeneo yote tunayopitia na bahati nzuri sababu mnajua kusoma na kuandika, mnayo fursa ya kujisomea na kujiongeza ili mpate hizo sifa,” amesema Prof. Juma.

Jaji Mkuu huyo wa Tanzania, amesema soko la ajira la sasa halihitaji vyeti vya taaluma pekee, bali linahitaji ujuzi wa ziada.

“Ninyi nyote mna sifa za kitaaluma ambazo zinahitajika, lakini hazitoshi katika ushindani wa sasa kukupa ajira. Karne ya 21 inataka zaidi ya vyeti, inataka ujuzi zaidi kutoka kwako. Ndiyo maana ajira chache zinazotokea mtafanyiwa usaili, wataomba watu 600 watachukuliwa 10 tu,” amesema Prof. Juma.

Prof. Juma amehoji “ sasa kama vyeti vinatosha kwa nini unafanyiwa usajili, sababu muajiri anatafuta ziada ambayo haiko kwenye vyeti, kazi kubwa mnayotakiwa kufanya ni kutafuta ziada ambayo haiko kwenye vyeti.”

Dk. Edward Hoseah, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS)

Amesema kinachokwamisha mawakili wengi kujiajiri, ni kutoruhusu mitazamo yao kubadilika na kuachana na dhana za kuajiriwa.

“Mawakili wengi hatujabadili mitizamo ili tuendane na mabadiliko katika soko la ajira, bado tunategemea kwamba Serikali na makampuni ya mawakili yatatoa ajira, lakini hayo makampuni yanapunguza watumishi na wanapunguza shughuli ambazo walakuwa wakitoa,”

“Katika maswali yangu kwa baadhi yenu nilitaka kujua kama mnafahamu dira ya maendeleo, wengi wenu hamfahamu ingawa huu ni mwaka wa 21 tangu hii dira ianze kufanya kazi. Hii inakupa sifa kwamba nchi yako inaelekea wapi, sasa kama hujui Tanzania inaelekea wapi hizo fursa huwezi kuziona,” amesema Prof. Juma.

Prof. Juma amewataka mawakili kusoma Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025, pamoja na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 hadi 2025/26, ili wajue Tanzania inaelekea wapi.

“Ni jukumu letu kuisoma hii dira na kuangalia inaweza ibua fursa gani, ambazo mawakili na wanasheria wanaweza kufanya. Changamoto kubwa kwenu vijana hamtaki kuelewa nchi yenu inakwenda wapi, wengi wenu wanaishia kulalamika,” amesema Prof. Juma na kuongeza:

“Ile dhana ya dunia inavyobadilika kwa kasi na sie tunatakiwa kubadilika hatuijui, ndiyo maana wengi wetu wanaishia kulalamika na kulaumu sababu wengine wanaona fursa lakini sisi hatutafuti nyenzo ya kuziona hizo fursa.”

error: Content is protected !!