August 8, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Jaji Lubuva kwisha zama zake

Jaji Semistocles Kaijage

Spread the love

JAJI Semistocles Kaijage ameteuliwa kumrithi Damian Lubuva aliyekuwa akiongoza Tume ya Taifa ya Uchaguzi – National Electoral Commission (NEC) – tangu mwaka 2011, anaandika Charles William.

Jaji Kaijage alikuwa mmoja wa majaji wa Mahakama ya Rufaa Tanzania, na uteuzi wake wa mkataba wa miaka mitano, unakuja katika wakati ambao tume haijaridhisha wakosoaji wake hasa kuhusu madai ya kupendelea Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichotangazwa mshindi wa uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka jana.

Taarifa ya Balozi John Kijazi, Katibu Mkuu Kiongozi aliyeko Ofisi ya Rais Ikulu), imesema Jaji Lubuva ambaye naye alitokea Mahakama ya Rufaa, amemaliza mkataba wa uteuzi wake uliofanywa 19 Disemba 2011 na aliyekuwa rais, Dk. Jakaya Kikwete, na kwamba Rais John Magufuli ameamua kuteua mtu wa kushika nafasi yake.

Balozi Kijazi amesema kwamba uteuzi wa Jaji Kaijage unaanza mara moja.

Jaji Lubuva ambaye alishastaafu ujaji, amekamilisha kuiandaa na hatimaye kuikabidhi ripoti ya uchaguzi mkuu uliopita kwa Rais Magufuli, lakini mpaka sasa wakosoaji wanasubiri kujua hasa kilichotokea kuhusiana na matokeo ya uchaguzi huo.

Wakati akitangaza matokeo ya uchaguzi wa rais mwaka jana, Jaji Lubuva alikuwa ameeleza kuwa matokeo hayo yametokana na taarifa za matokeo ya vituo vyote vya uchaguzi nchini na kwamba hakuna ubadhirifu wa matokeo uliotokea kama ilivyolalamikiwa na baadhi ya vyama vya siasa.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kililalamika kuwa matokeo yaliyotangazwa yalikuwa ya shaka kwa kuwa mgombea wake, Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, alitarajiwa kupata ushindi dhidi ya DK. Magufuli aliyesimamishwa na CCM.

Lowassa, kada aliyeingia upinzani akitokea CCM ambako alipigwa kumbo kwa staili iliyoitwa “amekatwa” akiwa mmoja wa waliokiomba chama hicho kuteuliwa kugombea urais. Wana-CCM wapatao 42 waliomba ridhaa ya CCM.

Matokeo ya uchaguzi wa urais yalitangazwa huku kukiwa na shutuma kali dhidi ya CCM kuwa ilikula njama ikitumia vyombo vya dola kulazimisha matokeo yanayokidhi matakwa yake ya kutaka kubakia madarakani.

Hata hivyo, Lowassa pamoja na Chadema na vyama vya Civic United Front (CUF), National League for Democracy (NLD) na NCCR-Mageuzi vilivyoungana katika mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), walilalamika kuhujumiwa kwa timu yao ya kukusanya matokeo ya kura za urais kutoka kwa mawakala wao vituoni nchi nzima.

Timu ya wanateknohama wa UKAWA ilivurugika baada ya ofisi zao kuvamia na Polisi na kukamatwa wakituhumiwa kufanya kazi ya kukusanya matokeo kinyume cha sheria.

error: Content is protected !!