January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Jaji Lubuva: Hakuna kura ya maoni

Spread the love

RAIS Jakaya Kikwete alikosea kutangaza tarehe ya upigaji kura ya maoni kuhusu Katiba Mpya inayopendekezwa. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Aliyepewa Mamlaka ya kutangaza tarehe ya upigaji kura ni “Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)”. Hii ni kwa mujibu wa Sheria ya Kura ya Maoni ya mwaka 2011, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2013.

Sheria hiyo inaitaka NEC kushauriana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kuhusu “ni lini na tarehe ipi kura ya maoni ipigwe”.

“Sheria ya Kura ya Maoni imezipa NEC na ZEC jukumu la kuendesha kura ya maoni kwa ajili ya Katiba Inayopendekezwa. Kwa mujibu wa Katiba na Sheria, tume hizi huendesha shughuli zake kwa uhuru bila kuingiliwa na mamlaka nyingine yeyote,” amesema Jaji Damian Lubuva- Mwenyekiti wa NEC.

Jumatano, 22 Oktoba mwaka jana, Vyombo vya habari viliinukuu taarifa kutoka Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu-Dar es Salaam ikisema, Rais Kikwete alitangaza rasmi kwamba, tarehe ya kura ya maoni ni 30 Aprili mwaka huu.

Aidha, Jaji Fredrick Werema – aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (CAG), aliyeng’oka 15 Disemba, 2014 kwa kashfa ya fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow, naye alivunja Sheria. Mwishoni mwa mwaka jana alitangaza kura ya maoni ingefanyika Machi 30 mwaka huu.

Kitendo cha Rais Kikwete na Jaji Werema kutangaza tarehe ya kupiga kura ya maoni kilizua maswali na sintofahamu kuhusu “Nani mwenye mamlaka ya kutangaza tarehe” kati ya Rais, Mwanasheria Mkuu na NEC.

Aidha, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Sheria ya Uchaguzi Sura ya 343 ya mwaka 2010, jukumu la NEC ni kusimamia na kuendesha uchaguzi wa Rais wa Tanzania, wabunge na madiwani wa Tanzania Bara.

Lubuva anasisitiza kwa kusema, “Tume inawataarifu kuwa zoezi lililotangazwa awali la Kura ya Maoni kufanyika 30 Aprili, 2015 limeahirishwa hadi tarehe itakapotangazwa na NEC baada ya kushauriana na ZEC”.

Lubuva ametoa nukuu hiyo leo jijini Dar es Salaam, wakati wa mkutano na waandishi wa habari.

Aidha, Lubuva amesema kura ya maoni itapigwa baada ya uboreshaji wa daftari la wapiga kura kukamilika Julai mwaka huu. Ambapo muda wowote kuanzia leo watapokea vifaa 248 na vingine kuletwa badaye kutoka nchini China.

Kauli ya Lubuva ya kufuta 30 April mwaka huu, kama tarehe ya kupiga “Kura ya Maoni” inakuja takribani saa 31 baada ya kuahirisha kikao cha Bunge mkutano wa 19 hapo jana.

Spika wa Bunge – Anne Makinda, alilazimika kuliahirisha baada ya mzozo uliotokana na mwongozo wa John Mnyika – Mbunge wa Ubungo (Chadema).

Myika alitaka Bunge liahirishe shughuli zake ili kujadili suala la dharura kuhusu uandikishwaji wapiga kura kwenye daftari kwa mfumo wa Biometric Voters Registration (BVR).

Wakati Mnyika akiendelea kujenga hoja yake, Spika Makinda alimzuia kwa madai kuwa hoja hiyo inafanana na hoja ya Mbunge wa Kisarawe – Suleiman Jaffo (CCM). Baada ya kauli hiyo ya spika ndipo ukaibuka mzozo.

error: Content is protected !!