Saturday , 20 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Jaji Bomani azikwa Dar, Majaliwa amwelezea
Habari Mchanganyiko

Jaji Bomani azikwa Dar, Majaliwa amwelezea

Spread the love

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa Kassim ameongoza mazishi ya aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hayati Mark Bomani huku akiwataka Watanzania wamuenzi kwa kuuishi utumishi wake uliotukuka wakati wa kupindi chote cha uhai wake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Majaliwa ameyasema hayo leo Jumatatu tarehe 14 Septemba 2020 wakati alipowaongoza waombolezaji kuuaga mwili wa Hayati Bomani viwanja vya Karimjee na baadaye katika mazishi yaliyofanyika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Majaliwa aliyemwakilisha Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema, Serikali imepokea msiba huo kwa huzuni na mshtuko mkubwa.

“Wote sisi ni mashahidi wa mchango mkubwa wa Mzee wetu Hayati Mark Bomani alioutoa katika tasnia ya sheria na katika nafasi mbalimbali alizotumikia ndani na nje ya Tanzania.”

“Alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa kwanza mzalendo, alisaidiana na Mwanasheria Mkuu wa kipindi hicho Roland Brown katika kutayarisha nyaraka zote za kisheria za Muungano.”

Majaliwa amesemma kati ya mwaka 1965 hadi 1976 aliteuliwa kushika nafasi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa kwanza mzalendo nafasi ambayo aliitumikia kwa uaminifu, uadilifu na umahiri mkubwa na alifanikiwa kufanya jitihada kubwa za kuhakikisha sekta ya sheria inaimarika.

Amesema Hayati Bomani aliwezesha kupatikana kwa Jaji Mkuu wa Tanzania kutoka nchini Trinidad and Tobago na Mahakimu kutoka Nigeria ili kupunguza uhaba wa watendaji Waafrika katika mhimili wa Mahakama.

Amesema Watanzania watamkumbuka Hayati Bomani kwa kazi kubwa aliyoifanya katika kamati mbalimbali zilizolenga kupitia sheria na keleta mabadiliko katika sheria.

Alikuwa Mjumbe wa Tume ya Rais iliyoundwa kutoa mapendekezo ya mfumo wa demokrasia wa chama kimoja.

Pia, Hayati Bomani alikuwa Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi, Mwenyekiti wa Tume ya Utangazaji, Mwenyekiti wa Kamati ya Kupitia Sera ya Madini ambayo iliwezesha kutungwa kwa sheria ya madini. Alikuwa mmoja wa Wajumbe wa Bodi ya Kwanza ya Udhamini ya CCM hadi umauti ulipomkuta.

Kadhalika, Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwasihi wanafamilia na waombolezaji wote waendelee kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo na kila mmoja kwa Imani yake wamuombe Mwenyezi Mungu ampumzishe Hayati Bomani mahala pema.

Hayati Bomani alizaliwa tarehe 2 Januari 1932 Bunda mkoani Mara na alikuwa kati ya watoto 10 wa Mzee Bomani.

Alisoma shule ya msingi Mwamanyili, Nassa ambapo baba yake mzazi ndiye alikuwa mwalimu wake.

Alipomaliza shule ya msingi alijiunga na shule ya Wavulana ya Bwiru Mkoani Mwanza ambapo alisoma hadi darasa la 10.

Alifaulu na kujiunga na shule ya sekondari ya wavulana ya Tabora na ambako pia alifaulu na kuchaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Makerere cha nchini Uganda mwaka 1953 hadi 1957 ambako alipata shahada ya kwanza ya masuala ya Siasa, Uchumi na Historia.

Mwaka 1957 hadi 1958 alijunga na Taasisi ya Ustawi wa Jamii ya The Hague na alitunukiwa diploma ya masuala ya jamii.

Mwaka 1958 hadi 1961 alijiunga na chuo Kikuu cha London nchini Uingereza na kutunukiwa shahada ya kwanza ya sheria.

Hayati Bomani mwaka 2019a aliugua na kupata matibabu nchini Afrika Kusini na India, hali yake ilikuwa nzuri na aliweza kurejea katika kazi alizozipenda za sheria lakini hali yake ilibadilika ghafla na alifariki dunia tarehe 10 Septemba 2020 na ameacha mke, Watoto watatu na wajukuu sita.

Mazishi hayo yamehudhuliwa na viongozi mbalimbali akiwemo Rais Mstaafu wa awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi na mkewe Mama Sitti, Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Mrisho Kikwete, Jaji Mkuu Mstaafu, Mohamed Chande Othman na Majaji wastaafu Damian Lubuva na Joseph Warioba.

Wengine ni Jaji Mkuu Mstaafu Barnabas Samatta na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

Wauguzi, madaktari 1000 kugawiwa mitungi ya Oryx Gas

Spread the loveKAMPUNI ya Oryx Gas na Taasisi ya Doris Mollel Foundation...

Habari Mchanganyiko

Tanzania yachaguliwa Makamu wa Rais Tume ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani

Spread the love  TANZANIA kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)...

Habari Mchanganyiko

NEMC yaonya wanaojenga bila tathmini ya mazingira

Spread the loveBARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC),...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB Pesa Akaunti yawavutia wakaguzi wa ndani Afrika

Spread the loveUbunifu wa bidhaa bora wa Benki ya NMB pamoja na...

error: Content is protected !!