September 25, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Jaji aruhusu Mbowe, wenzake kutotaja mashahidi wao

Spread the love

 

MAHAKAMA Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, imeridhia ombi la mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu, kutotaja majina ya mashahidi wake wane, kwa kile walichokieleza, “kulinda usalama wao.” Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Jaji wa mahakama hiyo, Mustapha Siyani, ameeleza kuwa mahakama yake, imekubaliana na maombi ya mawakili wa Mbowe na wenzake, kutotaja mashahidi wao kwa sasa.

Alikuwa akitoa maamuzi madogo kwenye shauri hilo la jinai, linalomkabili Mbowe na wenzake watatu; Halfan Bwire Hassan, Adamu Hassan Kasekwa maarufu kama Adamoo na Mohamed Abdillahi Ling’wenya, leo Ijumaa, tarehe 10 Septemba 2021.

Washitakiwa hao wanatuhumiwa

Alisema, mahakama yake, imekubali ombi hilo lililowasilishwa na wakili wa utetezi, Peter Kibatala, kutokana na ukweli kuwa huenda mazingira yakawa siyo rafiki kwa mashahidi hao kutajwa.

“….kulikuwa na maombi ya wakili Kibatala, kwa niaba ya washitakiwa chini ya kifungu cha 21 cha Sheria ya Uhujumu Uchumi, kwamba mahakama itoe kibali cha kutowataja mashahidi wa upande wa utetezi kwa sasa, ili kulinda usalama wao.

Akifafanua maombi hayo, Jaji Siyani alisema, “baada ya kupitia maombi hayo, mahakama imechambua maombi hayo, kwamba kutowataja mashahidi lazima kuwa na mazingira maalum. Wapo waliokuwa askari na kwamba serikali inaweza kuwafikia kabla ya kutoa ushahidi.”

Aliongeza, “nimepima hoja hii na mawazo yangu ni kwamba askari hata akiwa amestaafu, anaweza kufikiwa. Sioni tatizo kukubali ombi lake. Nakubali mashahidi wanne wanaopangwa kuletwa mahakamani wasitajwe isipokuwa kama washitakiwa watakutwa na kesi ya kujibu, wataitwa mahakamani.”

Mbali na mashahidi hao wanne, mahakama hiyo imeelezwa na upande wa utetezi, kwamba wamepanga kuwatumia mashahidi saba, akiwemo Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro; aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na Tumaini Chacha, ambaye ni mke wa mshitakiwa wa kwanza, Halfan Bwire Hassan.

Wengine, ni washtakiwa wenyewe – Bwire, Kasekwa, Lingwenya na Mbowe – na kwamba wote kwa pamoja wataeleza mahakama, wasivyohusika na tuhuma zinazotajwa na Jamhuri dhidi yao.

Katika shauri hili, upande wa utetezi umepanga kuita mashahidi wasiopungua 11, wakiwamo baadhi ya maofisa wa Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ) na watu wengine mbalimbali, wakiwamo wanasiasa.

Freeman Mbowe akiwasili mahakamani Kisutu

Kabla ya kufikia maamuzi hayo, kuliibuka mabishano makali kati ya mawakili wa upande wa utetezi na wale wa upande wa serikali, kuhusiana na hoja hiyo.

Akiwasilisha maombi hayo, Kibatala alisema, anaomba mahakama iwaruhusu kutoa majina ya mashahidi hao wanne, kwa sababu wanaweza kutishwa na taasisi za serikali, kwa kuwa miongoni mwao ni maofisa wa jeshi.

Hoja hiyo, ilipingwa na mawakili wa upande wa mashitaka, wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando, kwamba halina msingi wa kisheria.

Kufuatia hoja hizo, Jaji Siyani aliahirisha usikilizwaji wa shauri hilo kwa muda wa nusu, ili kupata nafasi ya kupitia hoja za pande zote mbili, kabla ya kutoa maamuzi.

Mara baada ya Jaji Siyami kurejea mahakamani, akaeleza kuwa kwa uelewa wake, katika kanuni ndogo za uendeshaji wa mahakama, hazisemi maombi ya ulinzi yaletwe kwa njia gani, kuandika au mdomo.

Alisema, kanuni ndogo ya 24 inatoa mamlaka kwa Mahakama kutoa amri ya ulinzi kwa mashahidi.

Naye Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ester Martin alisema, upande wa Jamhuri, umepanga kutumia mashahidi 24, akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz na aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi na Makosa ya Jinai mkoani Arusha, Ramadhani Kingai.

Kwa sasa, Kingai ni Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Dar ea Salaam.

Wakili Ester alisema, wamepanga pia kutumia vielelezo 19 vya maandishi, ikiwemo maelezo ya onyo ya washtakiwa wote wanne; hati za upekuzi na za kuwasilisha vielelezo, taarifa ya uchunguzi wa kisayansi, ripoti ya uchunguzi wa kimaandishi na ripoti ya uchunguzi wa kitaalamu wa kitengo cha uhalifu wa kimtandao (Cyber Crime).

Wakili huyo alisema, watatumia vielelezo visivyo vya maandishi (vielelezo halisi), ikiwemo vifaa vya Jeshi la Wanawanchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT); simu na laini za simu, silaha moja aina ya Pisto, risasi moja na maganda ya risasi mawili.

Mapema asubuhi, Mbowe na wenzake walisomewa maelezo ya awali na mashtaka upya, ambayo waliyakana kuyatenda.

Jaji Siyani ameahirisha kesi hiyo hadi Jumatano, tarehe 15 Septemba 2021, ambapo inatarajiwa kusikilizwa mfululizo.

Mbowe na wenzake, wanakabilia na mashitaka sita, ikiwamo kula njama za kufanya vitendo vya ugaidi. Shitaka hili, linawakabili washtakiwa wote. Wanadaiwa kulitenda kati ya tarehe 1 Mei hadi 5 Agosti 2020, katika mikoa ya Arusha, Morogoro na Dar es Salaam.

Freeman Mbowe na wenzake wakiwa mahakamani Kisutu

Shitaka jingine, ni kushiriki vikao vya kupanga njama za kutenda kosa la ugaidi, linalowakabili wote, wanalodaiwa kulitenda kati ya tarehe 1 Mei hadi 5 Agosti 2020, kwenye Hoteli ya Aishi mkoani Kilimanjaro.

Shitaka la kumiliki mali, ambazo zilipangwa kutumika katika vitendo vya ugaidi, linamkabili mshitakiwa mmoja (Bwire), huku shitaka la kutoa fedha Sh. 69,9000 (laki sita), kwa ajili ya kufadhili vitendo vya ugaidi, linamkabili Mbowe peke yake.

Kwa mujibu wa maelezo ya mashitaka, Mbowe na wenzake wanadaiwa kupanga njama za kufanya vitendo vya ugaidi, ikiwemo kutaka kumdhulu kimwili Sabaya; kulipua vituo vya mafuta na mikusanyiko ya watu ikiwemo masoko, katika mikoa ya Morogoro, Arusha na Mwanza.

error: Content is protected !!