January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Jaji aliikimbia Burundi afunguka

Makamu wa Rais wa Mahakama ya Katiba ya Burundi, Sylvere Nimpagaritse aliyetoroka nchini Braundi baada ya kutishiwa kifo

Spread the love

SYLVERE Nimpagaritse -Makamu wa Rais wa Mahakama ya Katiba ya Burundi aliyekimbilia, hatimaye ameongea kwa kirefu kuhusu sakata la kukimbia kwake.

Nimpagaritse aliyekimbia siku ya Jumatatu, amesema yeye pamoja na majaji wengine wa mahakama ya katiba walikuwa kwenye vitisho ili kumuhalalisha Rais Pierre Nkurunziza katika mipango yake ya kuingia madarakani katika muhula wa tatu.

“Ilikuwa ni uchaguzi pekee niliobakiwa nao kwani bila ya kumpa nafasi nyingine kuingia madarakani ningekuwa kwenye matatizo,” Nimpagaritse aliyasema hayo kwa kundi dogo la waandishi wa habari waliochaguliwa kuongea naye huko Kigali.

Ameongeza kuwa, ilibidi atoroke mamlaka na kuweza kufika mpakani baada ya Imbonerakure kumzuia.

Nimpagaritse amesema aliona maisha yake yapo hatarini baada ya vitisho kwani mahakama ya katiba ilipewa amri kutoa maamuzi yatakayompendelea Nkurunzinza.

“Tulikutana Aprili 30 kama majaji wa mahakama ya katiba ili kupitia vifungu vya sheria, Katiba na Mkataba wa Amani wa Arusha ili kuhakikisha kama Nkurunziza ana haki ya kuingia madarakani kwa mara nyingine na tukagundua hastaili.

“Baada ya hapo tukaenda nyumbani na kukubaliana turudi tena siku inayofuata ili kuweka sahihi, lakini jioni ya siku hiyohiyo, majaji wote walipigiwa simu na kupewa vitisho. Mei mosi majaji hao, walipoona vitisho vinaendelea waliamua kuweka sahihi kwa kumpendeea Nkurunziza kugombea kipindi cha tatu,” alisema.

Amefafanua kuwa, “ni wakati huu nilijiona nimetenda kosa la kutosaidia chama tawala na vibaraka wauaji wa Nkurunziza na hivyo nikaamua kupanga kutoroka.

Kwa mujibu wa jaji huyo, alipofika mpaka wa Kusini Magharibi ofisi ya Rusizi, alisimamishwa na polisi waliokuwa wanalinda mpaka na baada ya kugundua ni afisa wa serikali mwenye cheo cha juu, walimruhusu kupita.

Anasema kuwa, baadaye (Imbonerakure) wanamgambo wanaohusishwa na chama tawala, waliwataka polisi hao wasimruhusu.

“Niliwaona Imbonerakure wanawaamrisha polisi amabao wanafanya kazi kwa maagizo ya wanamgambo hao wakitahadharishwa kuwa kama wataniruhusu basi watakata vichwa vyao. Nikachukua uamuzi kutoroka kwa kujificha kwenye kizuizi cha magari na kutokomea na kujikuta Rwanda,” amesimulia.

Tatizo la Burundi sio la kikabila tena

Nimpagaritse kutoka kablila la Watusi, amesema kuwa matatizo katika nchi za Afrika Mashariki sio tena ukabila kwani Wahutu na Watusi wote kwa pamoja wamesimama kupinga hatua ya Nkurunziza kutawala kipindi cha tatu.

“Majaji wenzangu wote kwenye Mahakama ya Katiba ni Watusi na hawakukubaliana na uamuzi wa Nkurunziza. Hata ukiangalia maandamano wengi wao wanaoongoza maandamano ni Wahutu.

“Hata watu wakaribu wa Nkurunziza, ikiwa ni pamoja na msemaji wake wa zamani, wote walikuwa ni sehemu ya waandamanaji ni Wahutu. Kwa hiyo, kinachotokea hakina uhusiano na ukabila, badala yake wale wanaomuunga mkono Rais ndio wanaofanya ionekane kuwa matatizo haya ni ya kikabila na wanatumia kivuli cha maandamano hayo kuwa ni tatizo la kikabila ili wasilaumiwe kuwa wao ni chanzo.

Wakati akihutubia Taifa siku ya Jumatano, Rais Nkurunziza aliwataka wawe watulivu na kuwataka waandamanaji kusitisha maandamano ili kuruhusu maandalizi ya uchaguzi mkuu kwa amani.

Pia alisema kuwa hataendelea tena kwa kipindi cha nne endapo atachaguliwa kwa muhula wa tatu unaotarajiwa kufanyika Juni 26 mwaka huu.

Tangu fujo hizi zitokee tarehe 26 Aprili, watu 17 wamepoteza maisha ikijumuisha raia na askari. Kwa mujibu wa UNHCR, watu zaidi ya 50,000 wamekimbilia Rwanda, Tanzania na DRC.

Habari hii imetafsiriwa kutoka gazeti la The East African.

error: Content is protected !!