November 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Jacqueline Mengi ajitokeza ‘nawapenda’

Spread the love
MJANE wa hayati Dk. Reginald Mengi, Jacqueline Mengi amesema, mambo magumu wanayoyapitia wajane sasa na yeye anayapitia. Anaripoti Martin Kamote…(endelea).

Jacqueline ametoa kauli hiyo leo tarehe 26 Agosti 2019, alipotembelewa nyumbani kwake na Chama cha Wajane Tanzania (TAWIA).

“Nawashukuru sana kwa upendo, na mimi pia nawapenda. Naomba tuendelee kushirikiana na tuendelee kupendana, najua ninayoyapitia kwa sasa na nyinyi mmeyapitia,” amesema.

Mumewe Jacquelin, Dk. Rginald Abraham Mengi, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kampuni zilizo chini ya IPP na moja ya watu mashuhuri, alifariki dunia tarehe 2 Mei 2019 akiwa nchini Dubai, alizikwa kijijini kwao Machame, Kilimanjaro.

Rose Sarwatt, Mkurugenzi wa TAWIA amesema, lengo la kumtembelea Jacqueline nyumbani kwake, ni kumfariji kutokana na kutambua mateso ambayo anayapitia akiwa mjane.

“Tumekuja kumtia moyo, tunatambua msiba ule ulikuwa ni mkubwa na tulishiriki lakini hatukupata nafasi ya kuja kukaa naye na kumuonesha kwamba kundi hili ni kubwa, tumekuja baadhi tu na wamekuja watu wachache lakini tupo wengi.

“Kundi hili ni kubwa mno, linapitia changamoto kubwa ikiwemo kuhusishwa na mambo ambayo hatujafanya wala kuwaza kuyafanya. Kifo ni ajenda ya wote, hatuna haja ya kurushiana vidonge wala kuona kwamba huyu ameua au ameroga, hapana! kila mwanadamu aelewe kwamba ajenda ya kufa  ni ya wote,”amesema.

Sarwatt amesema, madhumuni ya kuanzishwa kwa TAWIA mwaka 2014, ni kuwaweka wajane pamoja, ili kutambuana, kufahamiana na kujua changamoto mbalimbali anazopitia mjane.

Pia, kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali wanazopitia ikiwemo kusomesha watoto, elimu ya sheria, afya, saikolojia, biashara na ujasiriamali.

Arone Mpole, Kiongozi wa wanaume waliofiwa na wake zao (wagane) ambaye aliambatana na wajane hao amesema, wanadamu wameumbwa kutiana moyo hivyo akiwa kama kiongozi wa wagane, amefika kwa ajili ya kuungana na kina mama hao kwa ajili ya kumtia moyo mjane mwenzao.

“Jacqueline ajue kwamba si pekeyake bali huko nyuma yake wapo wengi ambao waliyafika matatizo hayo, na pengine hao wengine yamewafika makubwa zaidi lakini kilichoweza kuwasaidia ni binadamu tunavyokusanyika na kusaidiana,” amesema.

error: Content is protected !!