BONIFACE Jacob, aliyevuliwa umeya wa Manispaa ya Ubungo, jijini Dar es Salaam, amesema taratibu zinamtambua kuwa bado ni Meya. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam…(endelea).
Mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo tarehe 8 Mei 2020, amesema mchakato uliotumika kumuondoa kwenye madaraka hayo, haukubaliki na ni haramu.
“Siku ya Jumamosi tarehe 2 Mei 2020, kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo aliutangazia umma, kwamba nimekosa sifa ya kuendelea kuwa Diwani wa Kata ya Ubungo na Mshatahiki Meya.
“Ni kwa kile kilichoitwa kuvuliwa uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), na mtu hewa. Asiyejulikana,” amesema Jacob.
Amesisitiza, kwa kuwa taratibu za kuvuliwa umeya zilizoainisha hazikufuatwa, yeye bado ni meya wa Ubungo na kwamba, barua iliyotumiwa kumvua uanachama ni ya kughushi.
“Barua hiyo haikuwa na muhuri wa ofisi au sehemu inapotoka, haina mawasiliano ya ofisi au mtu aliyeiandika, haijanukuu vifungu vya vya Katiba ya Chadema,” amesema Jacob.
Jocob amedai, kitendo hicho kimetekelezwa na watu wenye nia ovu baada ya yeye na baadhi ya madiwani wa chama chake, kuanika hadharani upotevu fedha za Halmashauri kiasi cha shilingi 1.6 Bilioni.
Jacob amesisitiza, kuwa taarifa zilizotolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Beatrice Dominic hazina ukweli.
Leave a comment