July 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Iyombe: Makazi kusajiliwa kisasa

Spread the love

 

SERIKALI imepanga kutumia mfumo wa rejesta ya makazi kwa njia ya kielektroniki ili kupunguza gharama, kutopatikana kwa taarifa sahihi pamoja na kupeleka huduma stahiki kwa wananchi wote, anaandika Regina Mkonde.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Injinia Mussa Iyombe, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI wakati akitoa maelezo juu ya mpango wa majaribio wa mfumo wa rejesta ya makazi kielekroniki unaofanyika katika Kata ya Mapinga wilayani Bagamoyo.

“Ofisi yangu ya TAMISEMI inaendelea kufanya juhudi za kuboresha mfumo wa upatikanaji wa taarifa sahihi katika ngazi ya kitongoji na mtaa kwa kuboresha mfumo wa daftari na kutumia teknolojia ya kisasa ili kuboresha upatikanaji wa takwimu bora katika serikali za mitaa,” amesema na kuongeza.

“Mfumo wa rejesta ya makazi kielektroniki utasaidia kupunguza gharama katika shughuli zinazofanyika serikalini, na pia mfumo huu utaipa fursa kubwa Ofisi yetu ya Takwimu kuwa na takwimu bora ambazo zitaipunguzia gharama ya tafiti za kila baada ya miaka mitatu na kuendelea.”

Injinia Iyombe amesema awali serikali ilikuwa inashindwa kupeleka misaada ya kijamii ya kutosha kwa wananchi hususan yanapotokea majanga hali iliyosababishwa na ukosefu wa taarifa sahihi za wakazi wa eneo husika.

“Nina imani kuwa hata Tume ya Uchaguzi watatumia kanza data hii kwa ajili ya kuboresha daftari la wapiga kura mwaka 2020, Wakala wa RITA, Vitambulisho vya Taifa na mazoezi mengine kama hayo ya kitaifa,” amesema

Amesema tathmini ya mfumo huo mpya itakapoanza kufanya kazi rasmi, itakuwa kila baada ya miezi mitatu kwa lengo la kuona changamoto na mafanikio yanayopatikana katika mfumo huu.

Ibrahim Mbonde, Diwani wa Kata ya Mapinga ambayo inafanyiwa majaribio ya mfumo huo kitekinolojia, amesema hadi sasa mfumo huo umeiwezesha kata hiyo kupata taarifa ya idadi kamili ya wakazi wake.

“Kaya 341 zimefanyiwa zoezi hili na kwamba limesaidia kutupatia taarifa sahihi sababu awali tulikuwa tunatumia madaftari ambayo ni rahisi kuharibika, vilevile hayajazwi taarifa hizo kwa wakati husika na pia yanatumika mengi na kwamba hutumia gharama kubwa tofauti na mfumo huu,” amesema.

Mbonde amesema mfumo huo utakapoanza kazi utasaidia kupunguza wahalifu kutokana na kwamba kila mwananchi atakayehama kutoka sehemu moja kwenda nyingine lazima apelike taarifa sahihi ya mahala anapotoka.

error: Content is protected !!