August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Itamchukua miaka Magufuli kueleweka Z’bar

Spread the love

RAIS John Magufuli ametanua wigo wa mayowe yake alipokuwa Zanzibar kwa ziara ya kilichoitwa ‘kuwashukuru wananchi kwa kumchagua,’ anaandkia Jabir Idrisa.

Baada ya kuwanyambua wananchi, hasa wa Pemba, na kwa jumla Wazanzibari wasiokiamini Chama Cha Mapinduzi (CCM) kama chama kifaacho kuwaongoza, Dk. Magufuli aliwatishia kwa kisingizio cha kulinda amani.

Rais anaamini Tanzania ina amani. Anaamini wanaoiharibu ni wapendao upinzani. Kwake, Watanzania wanaoshabikia CCM, ni watu wema sana. Hawana doa wala toa. Wasafi na wazalendo kuliko wapinzani.

Kwa bahati mbaya, katika kuwatisha Wazanzibari, hakuzungumzia “haki.” Hakusema, pengine kwa kutojua, kama amani inakwenda na haki. Hakueleza kama “HAKI” ndiyo huitengeneza “AMANI” na kwamba kwa maana hiyo, amani ni zao la haki.

Penye haki amani hustawi yenyewe. Kuinyima haki kwa anayestahiki, ni kudhulumu. Kwa hivyo, dhulma ndiyo msingi wa kuhatarishwa amani. Wale wananchi wanaodai haki iliyodhulumiwa, wanania njema. Wala hawahatarishi amani bali zaidi “wanatishiwa amani.”

Waliodhulumiwa wanakuaje na amani? Hawanayo. Wanaanzia wapi kuifaidi wakati wamedhulumiwa? Wanaohangaika kudai haki yao, ukweli wanatoa mchango wa kuijenga amani na kuidumisha. Bali wale wadhulumati ndio waihatarishao amani, ndio wavunjaji wa amani; ndio hasa wachochezi.

Tatizo la nchi za Afrika, na sasa Tanzania imeamua kujitumbukiza humo, viongozi wanaoshika madaraka, wameuzoea uovu mpaka sasa kuuona ni haki yao kuutendea dhidi ya watu wao. Ni mataifa machache yalipigana kudai haki baada ya uhuru mpaka walipokuja kugutuka kumekucha.

Nchi nyingi baada ya uhuru zilijengwa kwa sera za uimla (mabavu). Matokeo ya uongozi wa mabavu, ni wananchi kuwa woga kwa viongozi wao. Hakuna anayehoji wala kuuliza baada ya kiongozi kusema chochote. Uongozi usio mashauriano na majadiliano, ni uzandiki mtupu.

Uongozi huu uliotamalaki hata kuwazima raia kuhoji namna wanavyoongozwa, ndio uliozaa upinzani. Ilianzia na kuibuka kwa chembechembe za mabadiliko. Vikaja vikundi vya watu wanaohoji na kutaka waongozwe vizuri.

Kukawa na wimbi la mabadiliko. Lilianzia Ulaya ya Mashariki. Yalipotimia kwa Wajerumani wa Mashariki (waliokuwa chini ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ujerumani, GDR), kwa kufanikiwa kuuvunja ukuta wa Berlin, mwaka 1989, upepo ukatua Urusi.

Taifa hili lililokuwa na nguvu kubwa zilizoongoza kundi lililoitwa “Kambi ya Mashariki” baada ya kuunganisha nchi mbalimbali, likavunjikavunjika 25 Disemba 1991. Nchi zikarudi kwenye asili zao. Ndio leo kuwepo Russia na vijitaifa vile vidogo tele.

Sera za uimla zilizoshtadi na kusababisha ukandamizaji mkubwa wa haki za binadamu na haki za kiraia, zilibadilika alipoingia Mikhail Gorbachev. Aliichukua Urusi na kuibadilisha kupitia sera yake ya glasnost (uwazi) na perestroika (ujenzi mpya) ma kurahisisha kuvunjilia mbali Umoja wa Kisoshalisti wa Sovieti (USSR).

Matokeo hayo, yakaleta athari kwingineko duniani, kukiwemo barani Afrika ambako kulishakuwa na harakati nyingi za mabadiliko ya kukataa siasa za chama kimoja na kutakiwa mfumo wa vyama vingi.

Tanzania haikubaki salama na wimbi hilo. Baada ya wanasiasa waliojiamini kuibana serikali ya CCM kuacha ukiritimba wa madaraka, hatimaye Mwalimu Nyerere aliona hakuna namna ya kukwepa mfumo wa vyama vingi. Ingawa alishaondoka madarakani, alielekeza serikali ianzishe utaratibu wa kwenda na wakati.

Ndipo uongozi wa nchi chini ya Ali Hassan Mwinyi ulipounda Tume ya Jaji Nyalali na kuituma ikusanye maoni ya wananchi kuhusu haja ya kuendelea au kubadilisha mfumo wa siasa.

Hatimaye pamoja na walio wengi kutaka mfumo wa chama kimoja uendelee, wakajikuta wanalazimika kufuata kilichotakiwa na wachache – mfumo wa vyama vingi. Wao wengi waliutaka mfumo wa chama dola kushika hatamu, lakini kwa kuwepo marekebisho mbalimbali.

Tume ya Jaji Nyalali iliona kwamba kwa kuyarekebisha yale yaliyotajwa na walio wengi kama kasoro, mfumo wa chama dola, hautakuwepo tena. Marekebisho yatakuwa makubwa kiasi cha kuufumua mfumo mzima.

Rais Magufuli anapoizungumzia amani, atambue na haki waliyonayo wananchi katika maeneo mengi, likiwemo la kuchagua viongozi wawatakao. Anajua fika kwamba kwa Zanzibar, chama chao cha CCM kilikataliwa, ndio maana hata na mwenyewe alizidiwa kura.

Kiongozi alipata kura chache kuliko za Edward Lowassa, mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) aliyesimamishwa kwa mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kwa uchaguzi mkuu uliofanyika sambamba na ule wa Zanzibar tarehe 25 Oktoba 2015.

Kura za Lowassa kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), zilikuwa ni 211,033 kulinganisha na kura 194,317 alizopata Magufuli (asilimia 46.5).

Katika mwelekeo huohuo zilikuwa kura za wagombea wa urais wa Zanzibar, yaani CCM ilizidiwa na upinzani. Dk. Ali Mohamed Shein alipata kura 182,011 (asilimia 46.28) huku Maalim Seif Shariff Hamad wa Chama cha Wananchi akipata kura 207,847 (asilimia 52.84).

Kumbe ni nini basi kilitokea hata Dk. Magufuli leo alazimike kuhamasisha amani kwa vitisho huku akiwasimanga wananchi wa Zanzibar kwa kujionea wasivyoridhia uongozi wa Dk. Shein.

Hicho kilichotendwa kwa ridhaa ya viongozi wa CCM hata kubadilisha matakwa ya Wazanzibari kupitia utaratibu wa kikatiba, ndicho kinachowaweka roho juu wananchi wa Unguja na Pemba kwani kwa imani yao wanaamini wamedhulumiwa.

Kwa kudhulumiwa, maana yake wamenyimwa fursa ya kufaidi haki waliyoichuma kupitia visanduku vya kura Oktoba 2015. Nazungumzia unyimaji haki yao uliofanywa 28 Oktoba 2015 na hitimisho la usanii na ukatili lililoonekana 20 Machi 2016.

Kile kitendo cha nchi kumpata kiongozi kwa njia ya varange, ndicho kinacholalamikiwa Zanzibar. Na kwa kuwa Rais Magufuli amekiridhia kile, kwa kutochukua hatua kuwezesha haki kurejeshwa kunakostahiki, itamchukua miaka kurudisha amani myoyoni mwa Wanzanzibari. Siku zote amani hutanguliwa na haki na hudumu kwayo.

Makala hii imetoka katika Gazeti la MwanaHALISI la tarehe 12Septemba mwaka huu.

 

error: Content is protected !!