January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

ISUPILO: Kutoka mapumziko ya Mkwawa hadi gereza la kilimo

Mkuu wa Gereza Isupilo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP), Afulile Mwakijungu (kushoto) akiwa na maafisa wenzake shambani

Spread the love

 “ISUPILO ni neno la Kihehe, lenye maana ya eneo la kupumzika. Hapa ndipo yalikuwa mapumziko ya Chifu wa Wahehe, Mkwawa. Alikuwa akija hapa kupumzika.”

Haya yalikuwa maelezo ya utangulizi kutoka kwa Mkuu wa Gereza Isupilo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP), Afulile Mwakijungu kwa waandishi wa habari waliotembelea miradi ya magereza kujifunza utekelezaji wa program ya maboresho kwa wafungwa inayotekelezwa na jeshi hilo.

Gereza la Isupilo lipo Wilaya ya Mafinga mkoani Iringa. Inakuchukua umbali wa kilometa 13 kutoka Mafinga mjini.

Kwa mujibu wa SACP Mwakijungu, eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 10000.2 liligeuzwa matumizi kwa kujengwa gareza la kilimo Isupilo Agosti 4, 1971.

“Shughuli za uzalishaji katika gereza hili ni kilimo cha mahindi ya chakula- ekari 30 na mahindi ya mbegu bora aina ya Uyole High Bleed-UHB615 ambapo tumelima ekari 34.

“Pia tunazalisha mitamba (madume bora ya mbegu), tunaotesha mistu na kuhifadhi mazingira tukiwa na ekari 450 za mistu – ekari 50 ni miti aina ya mikaratusi ambayo hutumika kwa ajili ya kuni, mbao na nguzo za umeme,” anasema.

SACP Mwakijungu anaongeza kuwa, kama ilivyo miradi yote ya magereza sehemu mbalimbali nchini, pia wao wanatumia wafungwa kama sehemu ya maboresho ili kuwapatia ujuzi, pindi wamalizapo vifungo wajitegemee badala ya kurudia uhalifu.

Uzalishaji mitamba

Shughuli za ufugaji zilianza tangu gereza hilo lilipoanzishwa. SACP Mwakijungu anafafanua kuwa walianza wakiwa na majike ya kienyeji na madume bora ya kisasa ili kupata ‘mitamba chotara’.

“Lengo letu lilikuwa kupata kitoweo cha wafungwa pamoja na kuwauzia jamii iliyotuzunguka mitamba hiyo chotara,” anasema na kuongeza kuwa;

Kitaalam uwiano ni majike 25 hadi 27 kwa dume moja kwa mwaka mmoja. Kwamba shamba lao kwa sasa linayo madume 43 na majike 107 (sawa na ng’ombe 150), mbuzi 37, kondoo 67 na kuku wa kienyeji 47.

Kilimo

“Kama nilivyosema awali kwamba tunazalisha mahindi ya aina mbili- chakula na mbegu. Mahindi ya chakula tumeanza kuzalisha tangu gereza lilipoanzishwa – yemezalishwa mengi ya kutosha kulisha magereza yote ya mkoa wa Iringa,” anasema.

Kwa mujibu wa mkuu huyo, hali ya uzalishaji kwa sasa imebadilika kutokana na kutokuwa na zana za kisasa za kutosha. Anasema “kwa hapa tunahitaji tekta tatu lakini tunalo moja; ndio maana kwa msimu wa 2014/ 2015 tumeweza kulima ekari 30 badala ya 100.”

Kuhusu mahindi ya mbegu, anasema kilimo chake kilianza mwaka 2009 kwa lengo la kuzalisha mbegu bora kwa ajili ya wakulima wadogo.

Anasema “tunashirikiana na Wakala wa Taifa wa Mbegu (ASA) ambaye ni mnunuzi mkuu wa mahindi hayo. Hapa napo tulilenga kulima ekari 100 lakini tumeishia 34.”

Changamoto

SACP Mwakijungu anasema gereza hilo linahifadhi wafungwa wanaume wa vifungo virefu pamoja na mahabusu. Lakini anafafanua kuwa waofanya uzalishaji ni wafungwa pekee kwa sababu mahabusu hawapaswi kufanya kazi.

“Changamoto tuliyonayo ni idadi kubwa ya mahabusu kuliko wafungwa. Hapa ninao wafungwa 55 pekee ambao wanazalisha kulisha mahabusu zaidi ya 100 wanaohifadhiwa humu,” anasema.

Anasema kutokana na idadi ya wafungwa kupungua magerezani, serikali inapaswa kuwapatia pembejeo na zana za kisasa za kilimo za kutosha ili wafungwa wachache waliopo waweze kuzalisha kwa wingi kukidhi hitaji la mahabusu.

“Hata uzalishaji huu wa mahindi ya mbegu tunafanya lakini bado tunapunjika kwenye bei. Kwa mfano; tunanunua mbegu hizo kwa ASA, kilo Sh. 8,000 halafu baada ya kuzalisha tunamuuzia ASA huyohuyo kwa Sh. 1,000 kwa kilo,”anasema SACP Mwakijungu.

Kwa mjibu wa Mkuu wa Magereza Mkoa wa Iringa, SACP Isidore Mbuhe, mkoa huo una magereza nne ambapo mbali na Isupilo, mengine ni Gareza kuu Iringa, Pawaga na Mgagawa yanayojishughulisha na miradi mbalimbali.

“Gereza la Pawaga linajishughulisha na kilimo cha mpunga na ufugaji – Mgagawa wanashughulika na upandaji miti katika eneo hilo la zaidi ya ekari 600 lililokuwa likikaliwa na wapiganaji wa Afrika Kusini,” anasema SACP Mbuhe.

error: Content is protected !!