MIEZI sita baada ya kung’olewa Umeya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita amechukua fomu ya kuomba kuteuliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Anaripoti Hamis Mguta, Dar es Salaam … (endelea).
Isaya amejitokeza leo kwenye ofisi za chama hicho zilizopo Mtaa wa Ufipa, Kinondoni jijini Dar es Salaam, na kukabidhiwa fomu hiyo na Reginald Munisi, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa chama hicho.
Isaya alitangazwa kuvuliwa umeya tarehe 9 Januari 2020, kwa madai mbalimbali.
Miongoni mwa tuhuma zake ni pamoja na kushindwa kuongoza kikao cha baraza la madiwani na kupendelea baadhi ya mameya kuingia katika kamati za fedha.
Alituhumiwa kuwa na matumizi mabaya ya gari umma kwa kulisababishia kupata ajali, jambo ambalo meya amekuwa akijibu kwamba yeye siyo dereva wa gari hilo.
Lakini pia kutotumia kiasi cha Sh. 5.8 bilioni, zilizotokana na mauzo ya hisa za Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), ambalo lilikuwa mali ya jiji.

Isaya amechukua fomu leo tarehe 9 Julai 2020, Makao Makuu ya Chadema, Mtaa wa Ufipa jijini Dar es Salaam.
Mara baada ya kuchukua fomu hiyo, Isaya amesema kitu cha kwanza kwenye utawala wake ni Katiba Mpya kwa manufaa ya Watanzania wote.
“Katiba Mpya ndio jambo la kwanza nitakaloanza nalo endapo chama changu kitaniamini na kunipitisha na hatimaye kuwa Rais wa Tanzania, Katiba itaheshimiwa na kila mtu” amesema Isaya.
Leave a comment