December 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

India vs China: India yaongeza ndege za kivita

Ndege ya kivita ya India

Spread the love

WAKATI hali ya sintofahamu kati ya China na India ikishika hatamu, India imenunua ndege tano mpya za kivita aina ya Rafale zilizo na uwezo wa kurusha makombora ya masafa marefu. Inaripoti mitandao ya kimataifa…(endelea).

Ndege hizo zilizotengenezwa na Kampuni ya Ufaransa ya Dassault Aviation, ziliondoka nchini Ufaransa Jumatatu iliyopita tarehe 27 Julai 2020 na kuwasili Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ambako zilitua kwa muda kisha zikawasili India.

Taarifa zaidi zinaeleza, India ina mpango wa kuongeza ndege zingine na kuwa, ndege hizo ni miongoni mwa makubaliano ya taifa hilo na Ufaransa ya kununua ndege 36 za kivita yaliofanyika mwaka 2016.

Serikali ya India imesema, iliamua kununua ndege 36 za kijeshi kwa haraka ili kuangazia upungufu wa jeshi lake la angani. India inahitaji ndege 42 iwapo itakabiliwa na vita dhidi ya China na Pakistan.

Serikali ya Delhi inafanya haraka kuimaraisha jeshi lake la anga, ambapo kwa muda mrefu limekuwa likitumia ndege za zamani za kisoviet.

Ndege aina ya Rafale zina uwezo wa kufanya vitu tofauti ikiwemo kusafiri umbali mkubwa ikiwemo kufanya mashambulizi ya angani na ardhini bila kukosa.

Wachambuzi wanasema, kuwasili kwa ndege hiyo kutalisaidia jeshi la angani la India ambalo limekuwa likikabiliwa na upungufu wa ndege za kikosi hicho.

India na China, mataifa mawili yenye idadi kubwa ya watu duniani yakiwa na vikosi vikubwa vya kijeshi na silaha za nyuklia, zimekuwa zikikosoana kwa uvamizi kwenye Jimbo la Himalaya.

Hivi karibuni Jeshi la India lilisema, takriban wanajeshi 20 walifariki katika makabiliano na China.

India imekuwa ikilalamika, kwamba maelfu ya wanajeshi wa China wanaingia kwa lazima eneo la bonde la Galwan huko Ladakh, katika eneo linalozozaniwa la Kashmir.

Taarifa zinaonesha kwamba, mapema Mei, vikosi vya China viliweka vyandarua na kuchimba mahandaki pamoja na kuweka vifaa vya kivita kilomita kadhaa ndani ya kile ambacho India inakichukulia kama eneo lake.

“Hali ni tete. China imeingia eneo ambalo wao wenyewe wanakubali kwamba ni la India. Hili limebadili kabisa hali ilivyo,” anasema Ajai Shukla, mtaalamu wa masuala ya kijeshi wa India ambaye alihudumu kama kanali jeshini.

error: Content is protected !!