September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

India, China ‘vitani,’wanajeshi 20 wauawa

Spread the love

WANAJESHI 20 wa India wameripotiwa kuuawa baada ya kushambuliwa na Jeshi la China mpakani Magharibi mwa Milima ya Himalaya. Inaripoti mitandao ya kimataifa…(endelea).

Taarifa ya Jeshi la India iliyotolewa tarehe jana 16 Juni 2020, imeeleza wanajeshi wake 17 wamejeruhiwa vibaya.

“Wanajeshi wetu wamefia kazini, jumla ya wanajeshi waliofariki ni 20,” imeeleza taarifa ya jeshi hilo iliyotolewa ikieleza tathmini ya kinachoendelea mpakani.

Majeshi ya India na China yanapambana kwenye eneo la Ladakh katika mpaka wa Tibet ambapo kila mmoja anadai eneo hilo ni mali yake, hata hivyo India imeeleza, itatumia nguvu zake zote kulinda eneo hilo kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Mvutano wa nchi hizo mbili umekuwa ukiibuka dhidi ya eneo hilo la Kilomita 3,500 ambalo Jumuia ya Kimataifa hazijaeleza kwamba lipo upande upi. Kila taifa linadai, eneo hilo ni miliki yake

Maelfu ya wanajeshi kutoka mataifa yote mawili, wakiwa na vifaa vya kijeshi yakiwemo mizinga, vifaru na makombora wameweka makazi kwenye eneo hilo.

Taarifa ya jeshi hilo imeeleza, Majeshi ya China yamekuwa yakivuka vizuizi pamoja na magari yao, wakipuuza maelezo yote yanayotolewa kutoka Jeshi la India.

Zhao Lijian, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China ameitupia lawama India, kwamba imekuwa ikivuruga mipaka iliyokuwepo tangu awali na hata kuingia maeneo ambayo si mamlaka yao.

“Majeshi ya India yamevuka mpaka na kuingia kwenye ardhi ya China kinyume cha sheria mara mbili siku ya Jumapili. Hilo ndio limesababisha China kujihami kwa mashambulizi

“Kwa mara nyingine, kwa unyenyekevu tunaomba India ifuate na kuzingatia mipaka, na iondoe majeshi yake. Wasivuke mipaka, wasitutibue na kufanya chochote kitachishawishi mapigano,” ameeleza Lijian.

Serikali ya Beijing imethibitisha, kwamba Jumatatu wiki hii kulikuwa na mapambano ya suo kwa uso na majeshi ya India katika eneo hilo la mpaka.

“Hili ni jambo baya zaidi, baya sana na itasababisha kutibua mazungumzo ambayo tayari yalianza kufanywa,” amesema D S Hooda, kamanda wa zamani wa India alipozungumza na aljazeera.

error: Content is protected !!