Friday , 19 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Ilemela kusogezewa karibu huduma jumuishi za kisheria
Habari Mchanganyiko

Ilemela kusogezewa karibu huduma jumuishi za kisheria

Spread the love

 

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro, ameweka jiwe la msingi kwenye jengo jumuishi la taasisi za kisheria linalojengwa eneo la Buswelu Wilayani Ilemela mkoani Mwanza. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza … (endelea).

Jengo hilo litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kuhudumia watumishi 70 wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mashtaka ya Taifa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.

Akizungumza mara baada ya kiweka jiwe la msingi, Waziri Dk. Ndumbaro amesema kuwa ujenzi wa jengo hilo utasogeza huduma za kisheria na utoaji wa haki karibu na wananchi hivyo mwananchi atapata huduma za kisheria sehemu moja na huduma za ustawi wa jamii na msaada kisheria.

Vile vile, ameongeza kuwa ujenzi huo utagharimu Sh 3.8 bilioni na unatumia fedha za ndani ambazo ni kodi za wananchi na huu ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ambayo inaitaka tasnia ya sheria nchini kuwapa wananchi haki ya kisheria kwa karibu, kwa haraka na kwa gharama nafuu.

Amesema kuwa Serikali itaendelea kujenga majengo jumuishi nchi nzima kwa kila mkoa ikiwa ni pamoja na kuweka miundombinu mbalimbali na kutumia mifumo ya TEHAMA katika kuhudumia wananchi kwa kuwa taasisi za kisheria ni taasisi za utoaji haki hivyo ni muhimu kuimarisha miundombinu husika.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Naibu Katibu Mkuu, Dk. Khatibu Mizungu amesema kuwa majengo jumuishi yameonesha faida ya kwa watumishi kwa kufanya kazi kwa pamoja na yanajenga mahusiano mazuri baina ya taasisi za kisheria.

Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Dk. Eliezer Feleshi amesema kuwa matumizi ya pamoja ya fedha yamefanyika kwa kutumia fedha za Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na za Ofisi ya Mashtaka ya Taifa ambapo fedha za Ofisi ya Mashtaka ya Taifa zimetumika kununua kiwanja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inagharamia ujenzi wa jengo hilo.

Jaji Dk. Feleshi amesema kuwa uwepo wa jengo jumuishi utawezesha huduma zinazotolewa kupatikana katika eneo moja kwa kuwa Ofisi hizi zinategemeana katika utoaji huduma za kisheria kwa wananchi na itapunguza gharama kwa wateja kwa kuwa watakuwa wanapata huduma mahali pamoja.

Akizungumza kwa niaba ya Mshauri Elekezi wa ujenzi wa jengo hilo kutoka Wakala wa Majengo Tanzania, Mkurugenzi wa Huduma za Ushauri, Msanifu Majengo Wencelaus Kizaba amesema kuwa hadi sasa mkandarasi wa jengo hilo, SUMA JKT tayari amelipwa Sh 885,422,794kati ya Sh. 3.8 bilioni na TBA ambaye ndiye mshauri elekezi amelipwa shilingi 32,468,435 na ujenzi umefikia kiwango cha asilimia 35% na ni wa muda wa miezi 18 ambapo hadi sasa imetumika miezi saba na mkataba umeingiwa tarehe 19 Aprili, 2022 na ujenzi unatakiwa kukamilika tarehe 25 Oktoba, 2023.

Amefafanua kuwa ujenzi umetoa ajira kwa watanzania, wanafunzi wamepata mafunzo kwa vitendo na ununuzi wa vifaa vya ujenzi unafanyika kwa kununua bidhaa kutoka soko la ndani hivyo Serikali inapata mapato

Akitoa salamu kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, ndugu Hassan Masala amesema kuwa uongozi wa Mwanza uko tayari kuendelea kusimamia ujenzi huo ili kuona ufanisi wa miradi mikubwa ya Serikali na watashirikiana na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria ili Serikali iweze kufikia malengo iliyojiwekea.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

NEMC yaonya wanaojenga bila tathmini ya mazingira

Spread the loveBARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC),...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB Pesa Akaunti yawavutia wakaguzi wa ndani Afrika

Spread the loveUbunifu wa bidhaa bora wa Benki ya NMB pamoja na...

Habari Mchanganyiko

Carbon First, Ruangwa wasaini makubaliano ya biashara ya hewa ukaa

Spread the love  KAMPUNI ya Carbon First Tanzania Limited na Halmashauri ya...

Habari Mchanganyiko

CBE yawakumbuka wenye mahitaji maalum Jangwani

Spread the loveCHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kimetoa msaada mbalimbali na...

error: Content is protected !!