June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ilala yatenda haki Migombani, Kata ya Segerea

Wakili Hella Mlimanazi akiwaapisha wajumbe wa Serikali ya Mtaa wa Migombani, Kata ya Segerea

Spread the love

SINEMA ya Mtaa wa Migombani, jimbo la Segerea, Wilaya ya Ilala, mkoani Dar es Salaam, imekamilika, anaripoti Pendo Omary.

Mamlaka ya serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo ilikumbwa na ulemavu, ikajivuta kwa kuwa imebanwa kuendeleza siasa za kihafidhina na dharau kwa utawala bora, ilisalimu amri.

Ingawa ilisimamia uchaguzi wa haki, uongozi, ambao imedhihirika pasina shaka kuwa ulibanwa na mzimu wa CCM wa ulevi wa madaraka, ilikuwa imegoma kutimiza wajibu wake wa haki wa kumuapisha kiongozi aliyechaguliwa na wananchi.

Kiongozi mwenyewe si mwingine isipokuwa Japhet Albert Kembo, Mwenyekiti mpya wa serikali ya mtaa huo ambaye alishaapishwa kwa utaratibu ulioandaliwa na wananchi wenyewe kupitia kwa Wakili wa Kujitegemea, Idi Msawanga, katika tukio lililofanyika nje ya ofisi za Mtaa zilizokuwa zimefungwa.

Ilikuwa sherehe fupi lakini iliyofanyika mbele ya viongozi wa Halmashauri hiyo ya Ilala pamoja na wakazi wa mtaa waliomsindikiza Kembo kulishwa kiapo ukumbi uleule waliolishwa kiapo viongozi wenzake 17 Januari.

Mwanasheria wa Manispaa ya Ilala, Hella Mlimanazi, aliongoza kiapo cha Kembo, kijana aliyepitishwa kugombea uongozi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Alishinda katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vitongoji na vijiji uliofanyika nchi nzima 14 Disemba mwaka uliopita, kwa kupata kura 547 ambazo hazikufikiwa na washindani wake wawili waliomfuatia – Uyeka Iddi Lumbyambya wa CCM (kura 273) na Mchatta Erick Mchatta wa Chama cha NCCR-Mageuzi (kura 205). Kura 1,024 zilipigwa, mbili zikiwa zimeharibika.

Kembo, mzaliwa wa Mtaa wa Msewe, jimboni Ubungo, Dar es Salaam, miaka 33 iliyopita, ameingia katika historia mpya maishani akionesha kijana mwenye msimamo imara wa kutambua kuibeba dhamana ya uongozi aliyopewa na wananchi waliomchagua.

Anathibitisha kuwa kiongozi mwelewa na jasiri kimsimamo kwa maneno yake, mara tu alipokula kiapo: “Nina furaha sana kukabidhiwa rasmi dhamana ya kuongoza wenzangu mtaa wa Migombani.”

“Sasa kwa vile nimethibitishwa na mamlaka husika kisheria kufanya kazi waliyonipa wananchi. Naenda kuanza kazi nikijua zipo changamoto nyingi lakini ni ndogo kwani wananchi wameniahidi ushirikiano wa kutosha.”

“Nilikuwa nina hamu sana ya kupata fursa ya kuwatumikia wakazi wenzangu wa Migombani, sema nilicheleweshwa hadi ikalazimu tuchukue msimamo mkali kubaki na haki yetu ya kuamua uongozi tunaoutaka,” alisema.

Akiwa ni mhitimu wa stashahada ya mipango na utoaji huduma sekta ya usafirishaji, Kembo, aliapishwa katika hafla iliyofanyika ukumbi maarufu wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Anatouglo, Mnazimmoja.

“Walinipa taarifa kwa mdomo jana jioni kupitia kwa Mtendaji. Niliambiwa nifike hapa mapema leo kwa ajili ya kuapishwa, barua yangu nitaikuta tu,” aliiambia MwanaHALISIonline.

Safu yote ya uongozi wa serikali ya mtaa wa Migombani, imeapishwa. Wengine ni Nyangeta Flora Justin, Rose Benard Mhagama, Anjelo Machunda, Ramadhani Rashid Seif na Paulina Mbalale.

Wakati uapishaji huo haukuwa na tatizo, mgogoro uliibuka pale Halmashauri ilipomleta Mariano Mauruli, kwa ajili ya kuapishwa kama mwenyekiti wa Mtaa wa Kigogo Fresh ‘B,’ Kata ya Pugu, jimboni Ukonga.

Mariano ambaye anatajwa kutangazwa mshindi isivyo halali kwa vile hesabu ya kura haikukamilika, alipigwa na wananchi waliofika kuzuia uapishaji wake.

Mwandishi wa MwanaHALISIonline alielezwa na wananchi kuwa wakati kazi ya kuhesabu kura ikiendelea, kituo cha uchaguzi kilivamiwa na makada wa CCM walipohisi Mariano anapoteza mbele ya mgombea wa Chadema, Patricia Mwamakula.

Makada hao walipora masanduku ya kura na baadaye taarifa za ndani zilizothibitishwa na ofisa wa polisi aliyekuwa kazini, zilisema kura zilichomwa moto mbele ya askari wa Jeshi la Polisi.

Gazeti limepewa matokeo na ofisi ya Manispaa zinazoonesha Mariano alipata kura 134, Patricia 127, Hassan Mfaume wa NCCR-Mageuzi tisa na Ramadhani Salum 17.

Polisi walimchukua Mariano na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi (Central) ambako aliandikisha malalamiko ya kushambuliwa. Alitafutiwa fulana mpya Kariakoo na kurudi Anatouglo ambako aliapishwa wakati wananchi walishaondoka.

error: Content is protected !!