January 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ikulu yaumbuka, Makanisa yawakana waliojiita wajumbe wake

Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Alex Malasusa akihutubia waumini wake

Spread the love

UCHAKACHUAJI katika uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, uliokanwa na serikali na chama tawala – CCM – sasa  unaweza kuthibitishwa, MwanaHALISI Online limeelezwa.

Jumuiya ya Kikristo nchini (CCT), imethibitisha kuwa wanaoitwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, kutoka madhehebu ya Kikristo hawakutumwa wala kuteuliwa na taasisi hizo.

“CCT ilipeleka mapendekezo ya wajumbe tisa kwa Rais wa Jamhuri. Kati ya hao, rais alimteua mjumbe mmoja tu, Bibi Esther Msambazi,” imeeleza taarifa ya CCT kwa vyombo vya habari.

Imesema, “Mjumbe huyu aliyeteuliwa ni mkristo wa kawaida (Lay Christian) na wala si kiongozi wa dhehebu lolote la wanachama wa CCT na pia siyo Mzee wa Kanisa analotoka. Ni Mkristo mwaminifu wa kawaida. Huyu ndiye mwakilishi wa CCT kwenye Bunge Maalum la Katiba.”

Jukwaa la Kikristo linaundwa na fungamo la majukwaa manne ambayo, ni Christian Council of Tanzania (CCT); Tanzania Episcopal Conference (TEC); The Council of Pentecostal Churches of Tanzania (CPCT) na The Seventh Day Adventist (SDA).

Taarifa hizi zimekuja miezi sita tangu Tundu Lissu aituhumu Ikulu ya Rais Jakaya Kikwete na chama chake, kwa kile alichoita, “Kuchakachua wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba.”

Lissu alidai ndani ya Bunge la Jamhuri kuwa baadhi ya wajumbe walioteuliwa kuingia katika Bunge Maalum la Katiba, hawakuteuliwa na taasisi zinazodaiwa kuwawakilisha, jambo linalothibitishwa sasa na CCT.

Katika tamko lake la jana, CCT inasema, “Viongozi wengine wa dini ya Kikristo (maaskofu na wachungaji) waliopo katika bunge hilo, hawakutumwa na CCT na wala CCT haina taarifa, ni vipi walichaguliwa kuwa wajumbe wa bunge hilo.”

Aidha, CCT imesema, haiwatambui viongozi wa kidini waliotoa tamko la kutetea Bunge Maalum la Katiba na mwenyekiti wake, Samwel Sitta, kwa kuwa madhehebu hayo hayana ndimi mbili.

“…misingi ya taasisi hizi kwa umoja wake, viongozi wakishakubaliana jambo fulani kwa pamoja na kwa umoja wao wanalisimamia na kulitekeleza. Ndiyo yao ni Ndiyo na Hapana ni Hapana.”

Limesema, “Kwa mantiki hiyo, CCT ikiwa mmoja wa taasisi zinazounda Jukwaa la Kikristo Tanzania, inaendelea kusisitiza kuwa msimamo wa viongozi wake ni kama ulivyotolewa na Jukwaa la Kikristo Tanzania kuhusiana na maoni waliyopeleka kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uenyekiti wa Jaji Joseph Warioba.”

Jukwaa linasema, “Matamko waliyotoa ni sahihi na itaendelea kuyasimamia na kuyasambaza hadi yamfikie kila mkristo ili wananchi wa Tanzania wapate Katiba wanayoitaka.”

Wameongeza, “Viongozi wa Jukwaa la Wakristo hawawezi kutafuta maoni ya viongozi wa dini walioko katika Bunge la Katiba kwa sababu hawawatambui kama wawakilishi wa taasisi zao na hivyo, kukataa kwa nguvu zote yale ambayo viongozi hao watakuwa wakiyasema.”

Wamewataka wahusika wajiulize, “Hivi sisi tumetumwa na tunamwakilisha nani humu bungeni?”

Tamko la madhehebu ya Kikristo limetolewa siku moja baada ya vyombo vya habari kuripoti, Othman Masoud Othman, mwanasheria mkuu wa serikali ya Zanzibar, kujitoa katika Kamati ya Uandishi wa Katiba.

Mwanasheria huyo mashuhuri Visiwani amejitoa katika kamati hiyo kwa kile alichoita, “Kinachoandikwa ili kipelekwe kwa wananchi, sicho ambacho wananchi walipendekeza.”

error: Content is protected !!