January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ikulu imempa Tendwa kazi siyo yake

John Tendwa

Msajili mstaafu wa Vyama vya Siasa Tanzania, John Tendwa

Spread the love

Jina la John Tendwa, aliyekuwa msajili wa Vyama vya Siasa nchini, limeibuka tena upya, likiwa limesheheni porojo.

Tendwa ametaka mjadala juu ya rasimu ya katiba mpya usitishwe. Amekwenda mbali kwa kumtaka aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, kuacha kuzungumzia rasimu ya Katiba Mpya kwa sasa.

Anasema, “Kwa kuwa rasimu tayari iko bungeni, hakuna sababu ya Jaji Warioba kuendelea kujadili rasimu, kwani kwa kufanya hivyo ni kuwachanganya wananchi.”

Hapa Tendwa ameonyesha sura mbili, huku anaonyesha jeuri chafu na ujasiri wa kidikiteta na Kule anaonyesha woga na kudhihirisha kuwa anatumikia matakwa ya watu fulani, tena wachache katika utawala.

Kutaka kunyamazisha waliopewa kazi ya kukusanya maoni; kuratibu na kuchambua, katikati ya wingu la upotoshaji wa kanuni, ni kutumikia matakwa ya kundi fulani.

Ni Tendwa huyu huyu aliyejiita “mlezi wa vyama vya siasa” – pamoja kuwa ofisi ya msajili siyo ofisi ya kulea vyama – aliondoka ofisini akitishia kufuta vyama.

Wakati anatisha vyama, Tendwa alikuwa anajua mamlaka ya ofisi ya msajili wa vyama ni kuandikisha vyama na ukarani basi!

Kauli ya Tendwa iliungwa mkono na Salva Rweyemamu, mkurugenzi wa mawasiliano ya Rais (Ikulu). Salva amenukuliwa akisema, “Hakuna sababu ya kuzungumzia rasimu ya katiba. Liachwe Bunge Maalum la Katiba lifanye kazi yake.”

Lakini John Tendwa, amesoma sheria, anajua sheria, ingawa aweza kutokuwa na uelewa wa sheria. Hivyo anajua kuwa mchakato wa Katiba Mpya ulianza kukwama pale serikali kupitia mwanasheria wake mkuu, Frederick Werema ilipobadilisha kinyemela vifungu vya sheria ya kwanza iliyounda Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Werema alinyofoa baadhi ya vifungu vya sheria hiyo, aliivuruga na kuamuru tume iliyoongozwa na waziri mkuu mstaafu, Jaji Sinde Joseph Warioba, kumaliza kazi yake baada ya kukabidhi Rasimu ya Kwanza ya Katiba.

Kabla ya sheria kubadilishwa, tume ya Katiba ilipewa uhai wa kusimamia hadi kura ya pili ya maoni ya Katiba Mpya.

Sheria ya awali iliweka wazi kazi na majukumu ya tume; mamlaka yake na mipaka yake; baada ya kazi ya kuwasilisha rasimu bungeni kukamilika.

Baadhi ya kazi za tume, ni pamoja na kutoa elimu ya uraia na kuelekeza wananchi kuhusu vifungu vya katiba. Nyingine, ni kwenda mbele ya Bunge la Katiba kueleza maudhui ya kilicho katika rasimu; malengo ya baadhi ya vifungu vya rasimu na sababu ya kile kilichopendekezwa.

Kila mjumbe wa tume alikula kiapo chake kupitia sheria hii. Kwamba tume itasindikiza mchakato wa Katiba Mpya hadi kura ya pili ya maoni itakapofanyika.

Uamuzi wa kubadilishwa sheria hii uliwakatisha tamaa wengi. Baadhi ya wajumbe waliokuwa tume wakiongozwa na Joseph Butiku na Prof. Mwesiga Baregu, walikaribia kuachia ngazi. Aliyewarudisha hadi kubaki mpaka mwisho, ni Rais Kikwete na Jaji Warioba mwenyewe.

Kuna taarifa kwamba Rais Kikwete alimpelekea ujumbe Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, wa kuwabembeleza Butiku na Prof. Baregu. Mkutano kati ya Sefue na wajumbe hao ulifanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Katika mkutano huo, Balozi Sefue aliomba Prof. Baregu na Butiku, kufuta uamuzi wa kujiuzulu. Akakiri kuwapo makosa ya kubadilishwa kifungu cha sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Akasisitiza uamuzi wao wa kujiuzulu ungesababisha katiba mpya kutopatikana katika kipindi hiki cha utawala wa Kikwete. Hatimaye wajumbe walikubali kubaki ndani ya tume, ingawa walijua kuwa “hakuna dhamira ya kuandika katiba mpya.”

Sheria ya mabadiliko ya katiba iliyokuwa tumaini la wananchi kupata katiba mpya bila vurugu; bila vijembe na bila matusi, ilipitishwa na Bunge la Jamhuri, Februari 2012.

Ni baada ya vuta ni kuvute ya 14 Novemba 2011, pale wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), walipoondoka bungeni kupinga walichoita, “kuburuzwa na serikali.”

Hatua nyingine katika kuvuruga mchakato wa katiba ilikuwa pale Rais Kikwete aliporuhusu Samwel Sitta kuwa mwenyekiti wa bunge hilo. Baada ya kuendesha bunge la Katiba, Sitta aliamua kugeuza bunge hilo kuwa mkutano wa chama chake.

Kikwete anamfahamu Sitta; uwezo na ujanja wake. Hivyo aliamua kumtumia. Ni Sitta aliyekuwa Spika wa Bunge la tisa la Jamhuri. Alimteua kwa kusudi maalum, bila shaka la kumtendea kazi aliyomnong’oneza; kwani alikwishamtema pale CCM ilipokuja na hoja ya spika mwanamke huku wakijua Sitta asingeweza kupata na sifa hiyo.

Mara alipochaguliwa kuwa mwenyekiti wa bunge hilo, Sitta alianza mkakati wa kubadilisha baadhi ya kanuni za kuendesha bunge hilo kwa kudai kuwa zimepitwa na wakati.

Kanuni ambazo Sitta alitaka kubadilisha, zilikuwa hata hazijaanza kutumika. Zilikuwa zimepitishwa takribani siku tatu zilizopita.

Akaendesha upendeleo wa wazi bungeni kwa kuruhusu wajumbe wa chama chake kushambulia wengine. Akaamuru kuzima mijadala yote yenye kudhoofisha msimamo wa CCM wa kung’ang’aniza muundo wa serikali mbili.

Sasa swali la kujiuliza ni hili: Nani mwenye mamlaka zaidi ya kuzungumzia rasimu kama siyo Warioba na tume yake? Nani aweza kuminya uhuru wa wananchi wa kujieleza? Nani aweza kusema Tendwa hakutumwa katika mradi huu?

Je, kama Tendwa hakutumwa, aliwezaje kuwataka wananchi ambao kodi zao zimepotelea katika eneo hilo wanyamaze?

error: Content is protected !!