WAKULIMA wa mpunga kutoka wilayani Mbarali mkoani Mbeya, Ihefu FC wameivunja rekodi ya Mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Yanga SC. ya kutofungwa mechi 50 kuanzia msimu uliopita na msimu huu wa 2022/2023. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mbeya … (endelea).
Yanga ambao walikuwa wageni mkoani Mbeya, walikuwa wakisherehekea kufikisha mechi 49 bila kufungwa na kujinafananisha na Klabu maarufu ya Arsenal inayoshiriki Ligi kuu Uingereza.
Hata hivyo, katika mtanange huo uliopigwa leo tarehe 29 Novemba, 2022, umewaduwaza mashabiki wa Yanga baada ya kukubali kichapo cha bao 2-1 kutoka kwa Ihefu ambao walikuwa wakiburuza mkia katika msimamo wa Ligi Kuu Bara.
Licha ya Yanga kuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 9 ambalo lilitiwa kimyani Yannick Bangala, Ihefu walikuja kwa kasi na kufanikiwa kuandika bao la kwanza kupitia kwa Never Tigere dakika ya 39 na Lenny Kissu dakika ya 62.
Pamoja na Mwalimu wa Yanga, Nasreddine Nabi kufanya mabadiliko ya wachezaji hususani katika safu ya kiungo, bado timu ya Ihefu ilicheza kwa kujilinda katika dakika zote 90 na kujihakikishia ushindi.
Kwa matokeo hayo, Yanga imebaki kileleni na pointi 32 pamoja na mchezo mmoja mkononi wakati Azam wakifuatia kwa kufungana pinti na Yanga lakini wakizidiwa kwa uwiano wa magoli ya kufungwa na kufunga.
Ihefu waliokuwa wanaburuza mkia kwa pointi 8, sasa wamefikisha pointi 12 baada ya kushuka dimbani mara 14.
Leave a comment