INSPEKETA wa Jeshi la Polisi (IGP) nchini Tanzania, Simon Sirro ameema, ili kupunguza mrundikano wa mahabusu vituoni, hawafungia kesi za madai na migogoro ya ardhi na jukumu hilo sasa linafanywa na mahakama. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
IGP Sirro amesema hayo leo Ijumaa tarehe 26 Februari 2021, mbele ya Rais John Magufuli, aliyefungua jiwe la msingi la ujenzi wa Kiwanda cha Ushonaji katika Bohari Kuu ya Jeshi la Polisi.
Pia, Rais Magufuli amezindua majengo ya ofisi, madarasa pamoja na bweni la wanafunzi, Chuo cha Taaluma ya Polisi, Dar es Salaam.
“Hatutaruhusu kufungua kesi za madai polisi, kesi za madai ziende moja kwa moja mahakamani na zile za migogoro ya ardhi na kufanya hivi mheshimiwa Rais, imepunguza mrundikano wa mahabusu,” amesema IGP Sirro.
Kuhusu suala la upepezi, IGP Sirro amesema “sisi tumejipanga kuhakikisha upelelezi wa kesi mbalimbali unamalizika mapema, kesi ndogondogo zinakwisha ndani ya miezi sita na kesi kubwa zinamalizika ndani ya mwaka mmoja.”
Inspekta huyo wa polisi, ametoa onyo kwa wahalifu hususan wanaotumia silaha akisema “awamu hii si ya kuendekeza matumizi ya silaha au ugaidi. Wale ambao hawataki kubadilika, tutawabadilisha na mtu akichukua bunduki yake nyumbani, aage kabisa kwani hatuna muhali na hili.”
Leave a comment