INSPEKTA Jenerali wa Polisi (IGP) nchini Tanzania, Simon Sirro amewataka wanasiasa waliokimbia nje ya nchi kwa madai ya kutishiwa usalama wa maisha yao kurejea nchini humo kwani kuna amani na yuko tayari kuwapa ulinzi. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
IGP Sirro ametoa kauli hiyo leo Alhamisi tarehe 19 Novemba 2020 jijini Dar es Salaam, wakati anazungumza na wanahabari kuhusu tathimi ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020.
Kauli hiyo ameitoa kipindi ambacho wanasiasa wawili wa upinzani, wameondoka Tanzania wakihofia usalama wa maisha yao.
Wanasiasa hao ni, Tundu Lissu, aliyekuwa mgombea urais wa Tanzania kupitia Chadema aliyekwenda Ubelgiji na aliyekuwa mgombea Ubunge Arusha Mjini kupitia chama hicho, Godbless Lema aliyeko Kenya.
“Nchi yetu ya amani na utulivu na kama wako nje warudi nchini kuna amani. Ni vizuri Watanzania wakaelewa kwamba, hili ni suala la mtu binafsi anaamua kusema tu. Kimsingi tukipata taarifa hiyo niko tayari kumpa ulinzi na familia yake, ataishi kwa amani,” amesema IGP Sirro.
Akizungumzia sakata hilo, IGP amesema licha ya juhudi zake za kuiandika barua Chadema kumtaka Lissu na wanasiasa wengine wa chama hicho wanadai kutishiwa maisha kuripoti ofisini kwake, wanasiasa hao hawakutoa taarifa badala yake walikwenda kulalamika kwenye balozi za mataifa ya nje.
“Niliandika barua kwa Chadema aje aseme anatishiwa na nani maana unaweza kutishiwa na mtu mwingine hayo ni mambo ya kawaida unatishiwa unaenda kutoa taarifa ubalozi badala ya polisi,” amesema IGP Sirro.
IGP Sirro amesema “Lema kwenye uchaguzi tumezungumza sana, lakini yeye anatishiwa kuuawa hakuna taarifa iliyotolewa Polisi. Huo ni mkakati wa kutuchafua. Sisi jeshi hatuna habari yoyote ya kutishiwa kwa mtu.”
Leave a comment