SERIKALI ya Tanzania na Rwanda, zimekubaliana kushirikiana katika kukabiliana na vitendo vya ugaidi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Hayo yamesemwa na wakuu wa Jeshi la Polisi wa mataifa hayo mawili, leo Jumatano tarehe 8 Septemba 2021, katika mkutano wa ujirani mwema, kwa ajili ya kujadili changamoto za uhalifu unaovuka mipaka.
Akizungumza katika mkutano huo, Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi Rwanda, IGP Dan Munyuza, amesema jeshi hilo litashirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi la Tanzania, katika operesheni za kuzuia ugaidi, ikiwemo kubadilishana taarifa.
“Ahsante IGP Sirro kwa kukubali mwaliko wangu, kila siku nitakumbuka kufanya kazi pamoja katika kuweka mikakati kulinda nchi zetu na ukanda wetu dhidi ya vitendo vya ugaidi,” amesema IGP Munyuza na kuongeza:
” Tunatakiwa kuja pamoja mara kwa mara kama vikosi vya Polisi kufanya oparesheni, kubadilishana taarifa na kufanya operesheni katika mipaka ya kuingilia dhidi ya ugaidi. Jeshi la Rwanda litaendelea kufanya kazi kwa ukaribu na ushirikiano.”
Naye Inspekta Jenerali wa Polisi, IGP Simon Sirro, amesema huu ni wakati sahihi kwa majeshi hayo kushughulikia changamoto ya ugaidi, kwani ni vigumu kumfahamu mtu mwenye nia ya kufanya vitendo hivyo.
“Tumekuwa tukikabiliwa na changamoto ya ugaidi, kama mwenzangu alivyosema mbele yenu. Ni muda sahhi kushughulika nao, hakuna namna ya kujadiliana na gaidi ni ngumu kuhukumu akili ya gaidi,” amesema IGP Sirro na kuongeza:
” Ni dhahiri kwamba tunatakiwa kuwa tahadhari popote tunapopata taarifa moja kwa moja tufanyie kazi hiyo taarifa na nina uhakika kupitia taarifa hizo tutafanikiwa.”
IGP Sirro yupo katika ziara ya kikazi nchini Rwanda, ambapo anafanya mazungumzo na maofisa waandamizi wa Jeshi la Polisi nchini Rwanda.
Leave a comment