INSPEKTA Jenerali wa Polisi nchini Tanzania (IGP), Simon Sirro amesema mwili wa Hamza Mohamed ambaye aliwaua watu wanne wakiwemo askari polisi watatu, utakabidhiwa kwa ndugu zake au utazikwa na halmashauri. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Tukio hilo lilitokea tarehe 25 Agosti 2021 katika makutano ya barabara ya Kinondoni na Kenyatta karibu na Ubalozi wa Ufaransa jijini Dar es Salaam.
Hamza anadaiwa kuua askari polisi kwa Bastola aliyokuwa nayo kisha akachukua silaha walizokuwa nazo na kuanza kufyatua risasi hovyo na kumuua mlinzi wa kampuni ya ulinzi ya SGA, Joseph Okotya Mpondo.
Askari polisi waliouawa ni; Miraji Khatib Tsingay, Emmanuel Keralya na Kangae Jackson ambao miili yote minne iliagwa jana Ijumaa, tarehe 27 Agosti 2021, katika viwanja vya Kurasini Polisi kisha kusafirishwa kila mmoja kwenda kuzikwa kwao.
Leo Jumamosi, IGP Sirro akizungumza jijini Dar es Salaam amesema, mwili wa Hamza wataukabidhi kwa ndugu zao kama watachelewa halmashauri watauzika huku akiwataka Watanzania kujifunza kwa kile alichokifanya kijana huyo.
“Mwili wa Hamza tutawakabidhi ndugu zake, kwani tayari sisi tumekwisha ufanyia kazi, lakini siku zikipita hawajaja kuuchukua halmashauri itakwenda kuuzika,” amesema
“Hiyo familia inajisikiaje, hiyo familia ya Hamza inajisikiaje, fikiria wewe ndiyo mama yake, baba yake, kuzaa kwake imetuletea baala Watanzania. Niwaombe Watanzania wengine wasituzalie watoto kama Hamza,” amesema.
Leave a comment