INSPEKTA Jenerali wa Polisi (IGP) nchini Tanzania, Simon Sirro amefanya mabadiliko ya baadhi ya makamanda wa polisi wa mikoa (RPC). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea)
Katika mabadiliko hayo, IGP Sirro amembadilisha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa kuwa Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani (trafiki) kuchukua nafasi ya Fortunatus Musilim ambaye anakwenda kuchukua nafasi ya Mutafungwa.
Taarifa iliyotolewa jana Alhamisi tarehe 3 Desemba 2020 na Msemaji wa Polisi Tanzania, David Misime ilielezea mabadiliko hayo ni ya kawaida.
Misime alisema, licha ya nchi kuwa shwari, polisi linaendelea na operesheni mbalimbali zikiwepo za kukamata wanaojihusisha na uharifu mbalimbali ikiwemo wanaojihusisha na dawa za kulevya na matukio ya unyang’anyi na uvunjifu wa majumba
Mabadiliko ya makamanda yanahusisha, aliyekuwa RPC wa Kinondoni, Edward Bukombe amehamishiwa makao makuu kitengo cha picha na video na nafasi yake imechukuliwa na Ramadhan Kingai ambaye awali alikuwa Mkuu wa Upelelezi (RCO) Mkoa wa Arusha.
Aliyekuwa RPC wa Lindi, Stanley Kulyamo amehamishiwa Shule ya Polisi Moshi kuwa Afisa Mnadhimu wa Chuo hicho na nafasi yake imechukuliwa na Mtatiro Kitinkwi ambaye awali, alikuwa Afisa Mnadhimu Shule ya Polisi Moshi.
Aliyekuwa RPC wa Tabora, Barnabas Mwakalukwa amehamishiwa makao makuu kuwa Afisa Mnadhimu katika Kamisheni ya Ushirikishwaji wa Jamii na nafasi imechukuliwa na Safia Omary Shomari ambaye alikuwa Afisa Mnadhimu namna moja makao makuu.
IGP Sirro amemhamisha Lucas Mkondya kutoka Idara ya Maendeleo na Milki makao makuu kuwa Kaimu Kamishna wa Fedha na Lojistiki na nafasi yake kuchukuliwa na John Gudaba.
Katika mabadiliko hayo, Mpinga Gyuumi amehamishwa kutoka kitengo cha Ufuatiliaji na Tathimini makao makuu ya polisi Zanzibar kuwa mkuu wa utawala na rasilimali watu makao makuu Zanzibar.
Aliyekuwa mkuu wa utawala nma rasilimali watu , Faustine Shilogile amehamishiwa kuwa Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) makao makuu ya Polisi Dodoma, kuchukua nafasi ya Charles Kenyella ambaye amestaafu utumishi wa jeshi la polisi kwa mujibu wa sharia.
Leave a comment