May 17, 2021

Uhuru hauna Mipaka

IGP Sirro: 2020 wasilaumu dola

Simon Sirro, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP)

Spread the love

INSPEKTA Jenerali wa Polisi nchini Tanzania (IGP), Simon Sirro amesema, kuna viongozi wa siasa wanaashiria shari kwenye kauli zao na kwamba, ‘kesho’ wasiilamu dola. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Amesema, tayari ameona baadhi ya viongozi hao wakizungumza maneno makali na kwamba, katika sheria za taifa hili hakuna aliye juu ya Katiba.

“Wao wanachozungumzia si uchaguzi wa amani na utulivu, sera yao ni ushari, sasa ninavyoona mazingira ya baadhi ya viongozi, sitaki kuwataja, Watanzania tunaona, sasa ukiona viongozi wanaanza na ushari, kesho wasilaumu vyombo vya dola,” amesema IGP Sirro wakati akihojiwa kwenye kipindi cha Dakika 45 cha ITV wiki hii

“Nimeona viongozi wa siasa wanazungumza mambo makali sana. Ninawaheshimu viongozi wote wa siasa katika ngazi zote lakini lazima sheria na kanuni zilizopo ziheshimiwe.”

IGP Sirro alisema “ukiangalia baadhi ya viongozi wanavyozungumza, unaona kuna ushari. Ushari wanauonesha wanaupeleka kwa washabiki wao wawe na ushari huo huo.”

Alisema, Watanzania wengi hawana mazoea na shida na hawataki shida zinazotokana na uchaguzi ambapo amesisitiza kwamba kuna maisha baada ya uchaguzi.

“Watanzania wengi hawataki shida, lakini uchaguzi utapita na tutaendelea kuishi na sisi tuna watoto, tuna wajukuu tuna nani. Tunataka nchi yetu iendelee kuwa na amani na utulivu.”

“Hii habari ya maneno ya kusema mimi nimeishasema nimemaliza, hakuna aliyeko juu ya sharia, Watanzania wengi wanapenda amani,” alisema.

Alisema, kwa kuwa ana dhamana ya ulinzi na usalama, wanaojiandaa kwa ushari wajue watawakabili kwa mujibu wa sheria na wanaozivunja sheria.

Mkuu huyo wa jeshi la polisi nchini alisema, Tanzania haiwezi kupata viongozi wazuri katika vurugu, bali watapatikana kukiwa na amani huku akisisitiza viongozi hao kuendelea kunadi sera zao kuliko kutafuta shari.

Tanzania itafanya uchaguzi wake mkuu wa kuwachagua madiwani, wabunge, wawakilishi na Rais wa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 28 Oktoba 2020.

error: Content is protected !!