August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

IGP amng’oa OCD Ukerewe

Ahmed Msangi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza

Spread the love

JESHI la Polisi nchini limemuondoa Ally Mkaripa, Mkuu wa Polisi (OCD) wa Wilaya ya Ukerewe, Mwanza katika nafasi hiyo kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka, anaandika Moses Mseti.

Mkaripa anatuhumiwa kutumia vibaya madaraka yake, ikiwemo kutumia gari la serikali kubeba wasanii pia vinywaji kwa ajili ya baa yake kinyume na taratibu za jeshi hilo.

Mkaripa ameondolewa Ukerewe ambapo amerudishwa Makao Makuu ya Polisi mkoani Mwanza akitarajiwa kupangiwa majukumu mengine.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa, katika mkesha wa mwaka mpya 2017 Mkaripa aliagiza baa zote wilayani humo kufungwa lakini aliruhusu baa yake kufanya kazi hadi asubuhi.

Mtandao huu umezungumza na Ahmed Msangi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza ambaye amekiri kuondolewa kwa Mkaripa wilayani Ukerewe.

Kamanda Msangi amesema kuwa, kilichofanywa ni mabadiliko ya kawaida ya Jeshi la Polisi kutoka Makao Makuu jijini Dar es Salaam chini ya Ernest Mangu, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP).

Pamoja na Mkaripa kuwa na tuhuma za rushwa katika uongozi wake na matumizi mabaya ya madaraka Kamanda Ahmed amedai kwamba, hatambui tuhuma hizo.

“Ni uhamisho wa kawaida, hizo taarifa unazosema sizifahamu ndio ninazisikia kutoka kwako, Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam ndio wamefanya mabadiliko hayo na hakuna tuhuma kama hizo,” amesema Kamanda Msangi.

error: Content is protected !!