December 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Idadi ya wagonjwa wa corona yapaa

Spread the love

WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu ametangaza ongezeko la wagonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona nchini kutoka 53 hadi 88 baada ya wagonjwa wapya 29. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Taarifa iliyotolewa na Ummy leo Jumatano Aprili 15, 2020, inaeleza wagonjwa hao wamebainika baada ya kutoka majibu ya sampuli zilizopimwa maabara Aprili 14 na 15, 2020.

Inaeleza kuwa wagonjwa wote ni Watanzania, kati yao 26 wapo Dar es Salaam, wawili Mwanza na mmoja mkoani Kilimanjaro.

“Wote wanaendelea na matibabu chini ya uangalizi wa wataalam wa afya. Ufuatiliaji wa watu waliokuwa karibu na wagonjwa hawa unaendelea,” amesema Ummy.

Inaeleza hadi leo watu 88 wamepata maambukizi kutoka watu 53 waliotolewa taarifa awali.

“Ongezeko hili la wagonjwa linajumuisha wagonjwa wapya sita waliotolewa taarifa mapema leo na Waziri wa Afya Zanzibar (Hamad Rashid). Aidha wagonjwa waliopona hadi leo ni 11 na vifo ni vinne,” anaeleza Ummy.

Ummy amesema Serikali inaendelea kuwataka wananchi kuchukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huo kama wanavyopatiwa elimu mara kwa mara kupitia njia mbalimbali.

“Katika kipindi hiki ni muhimu kwa wananchi kuepuka misongamano na mikusanyiko isiyokuwa ya lazima. Ninawasihi wananchi kuacha kutoa taarifa za upotoshaji juu ya ugonjwa huu kwa kuwa zinaweza kuzua taharuki katika jamii,” amesema Ummy.

error: Content is protected !!